Other Medjugorje Messages - list
Languages:
English,
Afrikaans,
العربية,
Български,
Беларуская,
Català,
Čeština,
Deutsch,
Español,
Français,
Hrvatski,
Italiano,
Kiswahili,
Latviešu,
Magyar,
Malti,
Nederlands,
Polski,
Português,
Română,
Русский,
Shqip,
Slovenčina,
Slovenščina,
Suomi,
Svenska,
Tagalog,
Tiếng Việt,
Українська,
زبان_فارسی
This category includes messages that are given on special occasions, such are messages given during meetings of Ivan's prayer group and messages to Mirjana, which are often given to her on the 2nd of each month (see article Mirjana's latest apparitions - Mary's anxiety for those far from God)
“Wanangu wapendwa, nawaalikeni tena kupenda na kutohukumu. Mwanangu, kwa mapenzi ya Baba aliye mbinguni, alikuwapo pamoja nanyi ili awaonyesheni njia ya wokovu, awaokoeni si awahukumuni. Na ikiwa mnataka kumfuata Mwanangu, msihukumu na mpende, kama vile Baba aliye mbinguni anavyowapenda ninyi. Hata wakati mnapoteseka sana, au mnapojikwaa chini ya msalaba, msikate tamaa, msihukumu, bali kumbukeni kwamba mnapendwa, na msifuni Baba aliye mbinguni kwa upendo wake. Wanangu, msiiache njia ninayowaongozeni. Msikimbie kwenye maangamizi. Kusali na kufunga itawapa nguvu zaidi ili mweze kuishi kama vile baba wa Mbinguni atakavyo; ili muwe mitume wangu wa imani na upendo; ili maisha yenu iwe na baraka ya wale mnaowaona; ili muwe kitu kimoja na baba aliye mbinguni na Mwanangu. Wanangu, huu ni ukweli wa pekee, ukweli uletao wongofu wenu na kisha wongofu wa wengine wote wasiojua maana ya neno kupenda. Wanangu, Mwanangu aliwapeni wachungaji: muwalinde, na muwaombee. Nawashukuru! ”
“Wanangu wapendwa, katika wakati huu wa wasiwasi nawaalikeni tena kutembea nyuma ya Mwanangu, na kumfuata. Nayajua maumivu, mateso na taabu zenu, lakini katika Mwanangu mtapumzika, ndani yake mtapata amani na wokovu. Wanangu, msisahau ya kuwa Mwanangu amewakomboa ninyi kwa msalaba wake akawajalieni kuwa tena wana wa Mungu na kuwafundisha kumwita tena "Baba" yenu, Mungu aliye mbinguni. Ili muwe wapenzi wa Mungu Baba, basi muwe na mapendo na msamaha, kwa kuwa Baba yenu ni upendo na msamaha. Salini na fungeni, kwa maana hii ndiyo njia ya kujua na kumfahamu Baba aliye mbinguni. Mtakapomjua huyo Baba, mtafahamu ya kuwa Yeye tu ni muhimu kwenu (Maria Mtakatifu amenena hayo kwa nguvu na amkazo sana). Mimi, nikiwa Mama, nataka wanangu wawe watu wenye umoja ambamo Neno la Mungu husikilizwa na kutekelezwa. Kwa hiyo, enyi wanangu, mfuateni Mwanangu, muwe kitu kimoja naye, muwe wana wa Mungu. Pendeni wachungaji wenu kama vile Mwanangu alivyowapenda alipowaita kuwatumikia ninyi. Nawashukuru! ”
“Wanangu wapendwa, kwa upendo wa kimama nawaomba mnipe mioyo yenu ili niweze kumtolea Mwanangu, ili naye aweze kuiokoa, kuiokoa kutoka uovu wote unaowafanya daima kuwa watumwa na unaowafanya kuwa mbali na ule Wema wa pekee, yaani Mtoto wangu, anayewaokoa kutoka yote yale yanayowaongoza kwenye njia ya uovu na kuwaondolea amani. Mimi natamani kuwaongoza kwenye uhuru wa ahadi za Mtoto wangu, kwa kuwa natamani hapa yatimizwe hasa hasa mapenzi ya Mungu, ili kwa kupatanishwa na Baba wa Mbinguni, kufunga na kusali, waweze kuzaliwa mitume wa mapendo ya Mungu, yaani mitume watakaoeneza kwa mapendo na uhuru, Mapendo ya Mungu kwa watoto wangu wote, mitume watakaoeneza mapendo aminifu kwa Baba wa Mbinguni na hivyo kufungua milango ya mbingu. Watoto wapenzi, toeni furaha ya mapendo yenu na mshikamano wenu kwa wachungaji wenu kama vile Mtoto wangu alivyowaomba wao kutoa furaha hiyo. Nawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa, tafadhali muelewe, muwe tayari wote, kwa matumaini makuu, kufungua mioyo yenu; hivyo mngeelewa yote, mngeelewa kwa upendo gani nawaiteni, kwa upendo gani nataka kuwageuza, ili kuwafurahisha, kwa upendo gani nataka kuwafanya wafuasi wa Mwanangu na kuwapa amani katika ukamilifu wa Mwanangu. Mngeelewa ukuu wa moyo wangu wa kimama, kwa hiyo, wanangu, salini, maana kwa njia ya kusali tu imani yenu hukua na upendo wenu huzaliwa, upendo ambao utapunguza uzito wa msalaba kwa maana hamtakuwa peke yenu kuubeba. Katika umoja na Mwanangu, tukuzeni jina la Baba wa Mbinguni. Salini, salini mpate tuzo la upendo, maana upendo ni ukweli wa pekee, upendo husamehe yote, hutumikia wote na kuwaona wote kama ndugu. Enyi wanangu, mitume wangu, udhamini ambao Baba wa Mbinguni amewawekeni, kwa njia yangu, mtumishi Wake, ni kitu kikubwa, ili kusaidia wale wasiomjua, kusudi zapatanishwe naye, kusudi wamfuate, kwa hiyo nawafundisheni kupenda, maana mkiwa na upendo tu mnaweza kumjibu. Nawaalikeni tena: pendeni wachungaji wenu, salini ili katika wakati huu wa shida jina la Mwanangu atukuzwe kwa njia ya mwongozo wao. Nawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa, nawapendeni, ninyi nyote, watoto wangu nyote, muwe wote moyoni mwangu, ninyi nyote mmepata upendo wangu wa kimama na ninatamani kuwaongoza nyote ili mjue furaha ya Mungu. Kwa hiyo nawaalikeni: nahitaji mitume wanyenyekevu ambao, kwa moyo mkunjufu, wanapokea Neno la Mungu na ambao wako tayari kuwasaidia watu wengine ili, kwa njia ya Neno la Mungu, waelewe maana ya maisha yao. Ili muweze kufanya hayo, wanangu, yawapasa, kwa njia ya kusali na kufunga, kusikiliza kwa moyo mkunjufu na kujifunza kujidhili au kujinyenyekesha. Yawapasa kujifunza kukataa yote yanayowatenganisha na Neno la Mungu na kutamani tu yanayowakaribisha. Msiogope, mimi nipo hapa. Ninyi si peke yenu. Namwomba Roho Mtakatifu ili awafanye wapya, ili awaimarishe. Namwomba Roho Mtakatifu, ili mkisaidia wengine, muweze kujiponya nyinyi wenyewe. Naomba ili, kwa njia yake, muwe wana wa Mungu na mitume wangu. ”
Kisha kwa mahangaiko makubwa Bikira Maria alisema:
“Kwa ajili ya Yesu, kwa ajili ya mwanangu, pendeni wale ambao Yeye aliwaita mkitamani baraka ya mikono ile ambayo Yeye tu ameyaweka wakfu. Msiyaruhusu maovu yatawale. Nawaalikeni tena: ni kwa njia ya wachungaji wangu tu moyo wangu utashinda. Msiyaruhusu maovu yawatenganisheni na wachungaji wenu. Nawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa! nawapendeni kwa upendo wa kimama, na kwa subira ya kimama nangojea upendo wenu na ushirikiano wenu. Nasali ili muwe jumuiya ya wana wa Mungu na wanangu. Nasali ili muweze kuwa jumuiya inayojihuisha kwa furaha na imani na upendo wa Mwanangu. Wanangu, nawakusanya kama mitume wangu na nitawafundisha jinsi ya kuwajulisha wengine upendo wa Mwanangu, na jinsi ya kuwafikishia habari njema, ambaye ni Mwanangu. Nipeni mioyo yenu iliyo wazi na iliyosafishwa, nami nitaijaza upendo wa Mwanangu. Upendo wake utaipa maisha yenu maana nami nitatembea pamoja nanyi. Nitakuwa pamoja nanyi hata tumfikie Baba wa Mbinguni. Wanangu, wataokoka tu wale ambao watatembea kwa upendo na imani kumwelekea Baba wa Mbinguni. Msiogope, nipo pamoja nanyi! Muwaamini wachungaji wenu kama Mwanangu alivyowaamini wakati alipowachagua, na muwaombee ili waweze kupata nguvu na upendo wa kuwaongozeni. Nawashukuruni. ”
“Wanangu wapendwa, kwa moyo wa kimama nawaalikeni tena kupenda, kusali bila kukata tamaa kwa zawadi ya upendo, kumpenda Baba wa Mbinguni zaidi ya yote. Mtakapompenda Yeye, mtajipenda wenyewe na jirani zenu. Mambo hayo hayawezi kutengana. Baba wa Mbinguni yumo katika kila mtu, hupenda kila mtu na kumwita kila mtu kwa jina lake. Kwa hiyo, wanangu, kwa njia ya kusali sikilizeni atakalo Baba wa Mbinguni. Ongeeni na Yeye. Muwe na uhusiano wa binafsi pamoja na Baba, atakayeufanya mkubwa zaidi uhusiano wake nanyi, jumuhiya ya wanangu, mitume wangu. Kama Mama napenda kwamba, kwa njia ya upendo kumwelekea Baba wa Mbinguni, inukeni juu ya ubatili wa malimwengu na muwasaidie wengine kujua na kumjongea polepole Baba wa Mbinguni. Wanangu, salini, salini, salini kwa zawadi ya upendo, kwa sababu upendo ndiye Mwanangu. Muwaombee wachungaji wenu, ili wawapende ninyi siku zote, kama vile Mwanangu alivyowapenda ninyi na kuonyesha akitoa maisha yake kwa wokovu wenu. Nawashukuruni. ”
“Wanangu wapendwa, kwa upendo wa kimama na uvumilivu wa kimama naona kutangatanga kwenu na kuendelea kupotea kwenu. Kwa sababu hiyo mimi nipo pamoja nanyi. Nataka kwanza kabisa kuwasaidieni kupata kujijua ninyi wenyewe, ili baadaye muweze kuelewa na kutambua yote yanayowazuia kujua bila unafiki na kwa moyo wote upendo wa Baba wa Mbinguni. Wanangu, Baba hujulikana kwa njia ya msalaba: kwa hiyo msikatae msalaba: kwa msaada wangu, mkafanye bidii kuuelewa na kuupokea. Mtakapoweza kuupokea msalaba, mtaelewa pia upendo wa Baba wa Mbinguni. Mtatembea pamoja na Mwanangu na mimi. Mtajipambanua na wale ambao hawakujua upendo wa Baba wa Mbinguni, kujitofautisha na wale wanaomsikiliza lakini hawamwelewi, na wale wasioenda pamoja naye, na wasiomjua. Mimi nataka ninyi mjue ukweli wa Mwanangu na muwe mitume wangu; ili, kama wana wa Mungu, muwe na mawazo yaliyo juu ya mawazo ya kibinadamu na siku zote na katika yote mkatafute kila mara mawazo ya Mungu. Wanangu, salini na fungeni ili muweze kuelewa yote ninayowaombeni. Muombee wachungaji wenu mkatamani kujua, mkishirikiana nao, upendo wa Baba wa Mbinguni. Nawashukuruni. ”
“Wanangu wapendwa! Ili mpate kuwa mitume wangu na kuweza kusaidia wale walioko katika giza, ili waweze kuujua mwanga wa upendo wa Mwanangu, mnapaswa kuwa na moyo safi na mnyenyekevu. Hamwezi kusaidia ili Mwanangu azaliwe na kutawala mioyoni mwa wale wasiomjua, iwapo Yeye hatawali moyoni mwenu. Mimi nipo pamoja nanyi, natembea pamoja nanyi kama mama, nabisha hodi katika moyo wenu, usioweza kufunguka bila ya kuwa mnyenyekevu. Mimi nasali, lakini salini nanyi pia, wanangu wapendwa, ili muweze kumfungulia Mwanangu moyo wenu safi na mnyenyekevu na hivyo kuweza kupokea vipaji nilivyowaahidi. Hapo ndipo mtakapoongozwa kwa upendo na nguvu za Mwanangu, hapo ndipo mtakuwa mitume wangu, ambao wanaweza kueneza kwa walio karibu yao matunda ya upendo wa Mungu. Kutokana na ninyi na kwa njia yenu Mwanangu atafanya kazi, maana mtakuwa na Yeye kitu kimoja. Moyo wangu wa kimama unatamani muungano wa wanangu wote, kwa njia ya Mwanangu. Kwa upendo mkuu nawabariki na kuwaombea wateule wa Mwanangu, wachungaji wenu, Nawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa! Kwa upendo wa kimama nataka kuwafundisha uadilifu, natamani kwamba katika kutenda kwenu kazi kama mitume wangu muwe wenye haki, maamuzi na hasa waadilifu. Natamani kwamba, kwa neema ya Mungu, muweze kupokea Baraka ya Mungu. Natamani, kwa njia ya kufunga na kusali, muweze kupata kutoka kwa Baba wa Mbinguni ujuzi, uhalali, utakatifu wa kimungu. Kwa ulinzi wa Mwanangu na wangu mtakuwa mitume wangu, ambao wanaweza kueneza neno la Mungu kwa wote wasiolijua, na mtaweza kushinda mapingamizi mtakayokutana nayo njiani. Wanangu, kwa njia ya baraka neema itawashukia, nanyi mtaweza kuilinda neema hiyo kwa kufunga na kusali, kwa kujitakasa na kujipatanisha. Mtakuwa na utendaji fanisi ninaohitaji kutoka kwenu. Waombeeni wachungaji wenu ili mionzi ya neema ya Mungu iangaze njia yao. Nawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa! Naja kwenu kama Mama na ninatamani kuwa kwangu kama Mama mtapata maskani, faraja na mapumziko. Kwa hiyo, wanangu, mitume wa upendo wangu, salini! Salini kwa moyo mkunjufu, utii na uaminifu kamili kwa Baba wa Mbinguni. Muwe na uaminifu, kama vile mimi pia nilivyokuwa mwaminifu nilipoambiwa ya kuwa nitachukua baraka za ahadi. Basi kutoka mioyo yenu yafike siku zote midomoni mwenu maneno haya "Utakalo lifanyike". Kwa hiyo muwe na uaminifu na salini, ili mimi niweze kuwaombeeni kwa Bwana, ili awape Baraka ya Mbinguni na kuwajaza Roho Mtakatifu. Hapo mtaweza kuwasaidia wale wote wasiomjua Bwana. Ninyi, mitume wa upendo wangu, mtawasaidia kumwita "Baba" kwa uaminifu wote. Salini kwa ajili ya wachungaji wenu na mujiaminishe katika mikono yao iliyobarikiwa. Nawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa! Kwa upendo wa kimama nataka kuwasaidia ili maisha yenu ya kusali na kutubu iwe juhudi ya kweli ya kumjongea Mwanangu na nuru yake ya kimungu, ili muweze kutengana na dhambi. Kila sala, kila Misa na kila mfungo ni juhudi ya kumjongea Mwanangu, msukumo kwa utukufu wake na kuepukana na dhambi. Ni njia ya muungano mpya wa Baba mwema na wanao. Kwa hiyo, wanangu wapendwa, kwa unyofu wa moyo uliojaa upendo mliite jina la Baba wa Mbinguni, ili awatie nuru ya Roho Mtakatifu. Kwa njia ya Roho Mtakatifu mtakuwa chemchemi ya upendo wa Mungu: kwenye chemchemi hiyo wale wote wasiomjua Mwanangu watakunywa, wote wenye kiu ya upendo na amani ya Mwanangu. Nawashukuru! Salini kwa ajili ya wachungaji wenu. Mimi nawaombee na nataka waonje siku zote baraka ya mikono yangu na tegemeo la Moyo wangu wa kimama. ”
“Wanangu wapendwa! Mimi, Mama yenu, nipo pamoja nanyi kwa ajili yenu, kwa mahitaji yenu na mafundisho yenu binafsi. Baba wa Mbinguni amewapa uhuru wa kuamua peke yenu na kujua peke yenu. Mimi nataka kuwasaidieni. Nataka kuwa Mama kwenu, mwalimu wa ukweli, ili kwa unyofu wa moyo wazi mjue usafi usio na mwisho, na mwanga utokao kwa hiyo ukweli ili kutawanya giza, yaani mwanga uletao tumaini. Mimi, wanangu, naelewa maumivu yenu na mateso yenu. Nani aweza kuwaelewa zaidi kuliko Mama mmoja! Lakini enyi wanangu? Mjue kuwa idadi ya wanaonielewa na kunifuata ni ndogo. Pia ni kubwa idadi ya waliopotea, hao ambao hawajajua ukweli ulio katika Mwanangu. Kwa hiyo, enyi mitume wangu, salini na tendeni kazi. Mbebe mwanga, msipoteze tumaini. Mimi nipo nanyi na hasa pamoja na wachungaji wenu. Nawapenda na kuwalinda kwa Moyo wa kimama, ili kusudi wao wanawaongozeni Paradisini alikowaahidia Mwanangu. Nawashukuru! ”
“Wanangu wapendwa! Nawaalika na kupokea ninyi nyote kama wanangu. Ninasali ili mnipokee na kunipenda kama Mama yenu. Nimewaunga ninyi nyote katika moyo wangu, nimeshuka katikati yenu na kuwabariki. Najua kwamba mnataka kwangu faraja na tumaini, kwa sababu nawapenda na kuwaombea. Nawaomba kujiunga nami katika Mwanangu na kuwa mitume wangu. Ili muweze kutenda hivyo nawaalika tena kupenda. Hakuna upendo pasipo sala, hakuna sala pasipo msamaha, maana upendo ni sala, na msamaha ni upendo. Wanangu, Mungu aliwaumba ili mpende, pendeni ili muweze kusamehe! Kila sala itokayo katika upendo huwaunganisha na Mwanangu na Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu awaangaze na kuwafanya mitume wangu: mitume ambao, kila watendalo, watalifanya kwa jina la Bwana. Wao watasali kwa matendo na siyo kwa maneno tu, kwa maana wanampenda Mwanangu na kufahamu njia ya ukweli iongozayo kwenye uzima wa milele. Waombeeni wachungaji wenu, ili waweze kuwaongoza daima kwa moyo safi katika njia ya ukweli na upendo, ndiyo njia ya Mwanangu. Nawashukuru! ”
“Wanangu wapendwa! Mimi Mama yenu, ninyi mliokusanyika hapa na Mama wa ulimwengu mzima, nawabariki kwa baraka ya kimama na kuwaalika kuanza safari katika njia ya unyenyekevu. Njia hiyo inawaongoza katika ujuzi wa upendo wa Mwanangu. Mwanangu ni Mwenye uwezo. Yeye yumo katika kila kitu. Kama ninyi, wanangu, hamelewi hayo, basi mtambue kuwa katika roho yenu giza na upofu zinatawala. Unyenyekevu tu huweza kuwaponya. Wanangu, mimi nilikuwa nimeishi daima kwa unyenyekevu, kwa uhodari na kwa matumaini. Nilijua, nilikuwa nimeelewa ya kuwa Mungu yu ndani yetu na sisi ndani ya Mungu. Nawaombeni kuelewa vile vile. Nataka ninyi nyote muwe pamoja nami katika umilele, maana ninyi ni sehemu yangu. Katika njia yenu nitawasaidia. Upendo wangu utawafunika kama joho na kuwafanya ninyi mitume wa mwanga wangu, wa mwanga wa Mungu. Kwa upendo utokao katika unyenyekevu, mtaleta mwanga palipotawala giza na upofu. Mtaleta Mwanangu, aliye mwanga wa ulimwengu. Mimi ni sikuzote kando ya wachungaji wenu na kusali ili wawe siku zote kwenu mfano wa unyenyekevu. Nawashukuru! ”
“Wanangu wapendwa! Sababu ya kukaa kwangu pamoja nanyi, utume wangu, ni kuwasaidieni ili wema ushinde, hata kama kwa sasa haya yaonekana ni kitu kigumu sana. Najua kwamba mambo mengi hamyaelewi, kama vile sikuelewa mengi ambayo Mwanangu alinifundisha akiwa alipokua pamoja nami, lakini mimi nilimsadiki na kumfuata. Haya nawaombea ninyi pia, kunisadiki na kunifuata, lakini, wanangu, kunifuata maana yake ni kupenda mwanangu kuliko wote, kumpenda katika kila mtu pasipo ubaguzi. Ili kuweza kufanya haya yote nawaalikeni tena kujinyima, kusali na kufunga. Nawaalikeni ili maisha ya roho yenu yawe ni Ekaristi. Nawaalikeni muwe mitume wangu wa mwanga, ambao wataueneza upendo na rehema ulimwenguni. Wanangu, maisha yenu ni mpigo tu wa moyo mbele ya uzima wa milele. Mtakapokuwa mbele ya Mwanangu, Yeye ataona katika mioyo yenu kiasi cha upendo mliokuwa nao. Ili kuweza kueneza kwa njia ya haki upendo nitamwomba Mwanangu kusudi kwa njia ya upendo awapeni umoja kati yenu na umoja kati yenu na wachungaji wenu. Mwanangu daima anajitoa upya kwa njia yao na anafanya mioyo yenu mipya. Msisahau hilo. Nawashukuru! ”
“Wanangu wapendwa, mimi, Mama yenu, naja tena katikati yenu kwa upendo usio na mwisho, kutoka upendo usio na kipimo wa Baba wa Mbinguni asiye na mwisho. Na, nikitazama mioyoni mwenu, naona ya kuwa wengi wenu wanipokea kama Mama na, kwa moyo thabiti na safi, wataka kuwa mitume wangu. Lakini Mimi ni Mama pia wa ninyi ambao hamnipokei na, katika ugumu wa moyo wenu, hamtaki kujua upendo wa Mwanangu. Hamjui jinsi moyo wangu ulivyoteseka na jinsi nilivyowaombeeni Mwanangu. Namwomba aponye roho yenu, kwa maana najua Yeye ana uwezo wa kuwaponya. Namwomba awaangaze kwa mwujiza wa mwanga wa Roho Mtakatifu, ili mwache kumsaliti, kumtukana na kumwumiza siku zote kwa kuendelea. Nasali kwa Moyo wote ili muweze kuelewa ya kuwa Mwanangu tu ni wokovu na mwanga wa ulimwengu. Nanyi, wanangu, mitume wangu wapenzi, mbebeni daima Mwanangu katika moyo na fikira zenu. Hivyo ninyi mtakuwa mnabeba Upendo. Wale wote wasiomjua watamtambua katika upendo wenu. Mimi nipo sikuzote karibu yenu. Nipo hasa karibu na wachungaji wenu, kwa sababu Mwanangu aliwaita kuwaongozeni katika njia kuelekea milele. Nawashukuru, mitume wangu, kwa sadaka na upendo wenu! ”
“Wanangu wapendwa, kwa upendo wa kimama nawaombeni: pendaneni! mioyoni mwenu muwe kama Mwanangu alitaka tangu awali: kwanza kabisa kumpenda Baba wa Mbinguni na kuwa na upendo kwa jirani yenu, kuliko yote yaliyopo hapa duniani. Wanangu wapendwa, hamtambui dalili za nyakati hizi? Hamtambui ya kuwa yote yanayotokea kando kando yenu, hutokea kwa sababu hakuna upendo? Fahamuni kwamba wokovu hupatikana katika thamani za kweli, pokeeni uweza wa Baba wa Mbinguni, mpendeni na kumheshimu. Fuateni njia ya Mwanangu. Ninyi, wanangu, mitume wangu wapenzi, mnakusanyika siku zote daima kunizunguka maana mna kiu, mna kiu ya amani, ya upendo na ya furaha. Kateni kiu yenu katika mikono yangu! Mikono yangu yawatolea Mwanangu, aliye chemchemi ya maji safi. Yeye atafufua imani yenu na kusafisha mioyo yenu, kwa sababu Mwanangu hupenda kwa moyo safi na mioyo iliyo safi humpenda Mwanangu. Mioyo safi tu ndiyo minyenyekevu na yenye imani thabiti. Wanangu, nawaombeni ya kuwa na mioyo ya namna hii! Mwanangu aliniambia ya kuwa Mimi ni Mama wa ulimwengu wote: nawaombeni ninyi, mnaonipokea kama Mama, ili kwa maisha yenu, sala na sadaka nisaidieni ili wanangu wote wanipokee kama Mama, niweze kuwaongoza kwenye chemchemi ya maji safi. Nawashukuru! Wanangu wapenzi, wachungaji wenu wanapowatolea mwili wa Mwanangu, mshukuruni Mwanangu daima moyoni mwenu kwa sadaka yake na kwa wachungaji anayewajalia siku zote. ”
“Wanangu wapendwa, mimi nipo pamoja nanyi kwa baraka ya Mwanangu, pamoja nanyi mnaonipenda na mnaotafuta kunifuata. Mimi natamani kuwa pia pamoja nanyi ambao hamtaki kunipokea. Kwenu nyote nafungua moyo wangu wote wa mapendo na kuwabariki kwa mikono yangu ya kimama. Mimi ni Mama ninayewaelewa: nilikuwa nimeishi maisha yenu na kujaribu mateso na furaha yenu. Ninyi mnaoishi katika mateso, mnafahamu maumivu yangu na mateso yangu kwa ajili ya wale wanangu wasiokubali kuangazwa na mwanga wa Mwanangu, kwa wale wanangu wanaoishi gizani. Kwa hiyo nawahitaji ninyi, ninyi mlioangazwa na mwanga na kuufahamu ukweli. Nawaalika kumwabudu Mwanangu, ili moyo wenu ukue na kuyafikia kweli maisha ya kiroho. Basi mitume wangu, natumaini mtaweza kunisaidia. Kunisaidia maana yake ni kuwaombea wale ambao hawajajua upendo wa Mwanangu. Mkiwaombea, mtamwonyesha Mwanangu ya kuwa mnampenda na kumfuata. Mwanangu aliniahidi kwamba uovu hautashinda kamwe, kwa sababu hapo mpo ninyi, roho za wenye haki: ninyi mnaojaribu kusali sala zenu kwa moyo wote; ninyi mnaotolea maumivu na mateso yenu kwa Mwanangu; ninyi mnaofahamu ya kuwa maisha ni kufumba na kufumbua tu; ninyi mnaotamani Ufalme wa mbinguni. Hayo yote huwafanya muwe mitume wangu na kuwaongoza kwenye shangwe ya Moyo wangu. Kwa hiyo wanangu, takaseni mioyo yenu mkamwabudu Mwanangu. Nawashukuru! ”
“Wanangu wapendwa, zingatieni akilini, kwa maana nawaambia: upendo utashinda! Najua ya kuwa wengi wenu wanapoteza matumaini kwa kuwa wanaona wamezungukwa na mateso, maumivu, husuda na wivu, hata hivyo mimi ni Mama yenu. Mimi nipo katika Ufalme, lakini hata hapa nipo pamoja nanyi. Mwanangu ananituma tena ili niwasaidieni, kwa hiyo msipoteze matumaini ila nifuateni, kwa maana ushindi wa Moyo wangu ni kwa jina la Mungu. Mwanangu mpendwa anawafikiria, kama alivyofanya siku zote: mwaminini na mwishi kama Yeye! Yeye ni uzima wa ulimwengu. Wanangu, kumwishi Mwanangu maana yake ni kuishi Injili. Si kitu rahisi. Ni jambo linalodai upendo, rehema na sadaka. Hayo huwatakasa na kufungua Ufalme: Sala nyofu, isiyo maneno bali itokayo moyoni, itawasaidieni. Vivyo hivyo kufunga, maana hayo huleta ongezeko la upendo, rehema na sadaka. Kwa hiyo msipoteze matumaini, ila nifuateni. Nawaomba tena msali kwa ajili ya wachungaji wenu, ili wamtazame daima Mwanangu, aliyekuwa Mchungaji wa kwanza wa ulimwengu, na ambaye familia yake ilikuwa ulimwengu wote. Nawashukuru! ”
“Wanangu wapendwa, nipo hapa katikati yenu kama Mama atakaye kuwasaidia kuujua ukweli. Nilipokuwa nikiishi maisha kama yenu duniani, nilikuwa nikijua ukweli na kwa hivyo kuwa na kipande cha Mbinguni duniani. Kwa hiyo, wanangu, nataka ninyi pia muwe washiriki wa hali hivyo. Baba wa Mbinguni ataka mioyo minyofu, ijaayo ujuzi wa ukweli: Ataka muwapende wote mnaokutana nao, maana mimi pia nampenda Mwanangu katika ninyi nyote. Huo ndio mwanzo wa ujuzi wa ukweli. Mtapewa kweli nyingi za uongo. Mtazitambua kwa mioyo iliyotakaswa kwa kufunga, kusali, kwa kufanya toba pamoja na kuishika Injili: Huo ndiyo ukweli wa pekee, nao ni ule ambao Mwanangu aliwaachieni. Msiufanyie utafiti mwingi sana: mnaombwa kuupenda na kuutoa, kama vile nilivyofanya mimi pia. Wanangu, mkipenda, mioyo yenu itakuwa maskani ya Mwanangu na yangu, na maneno ya Mwanangu yatakuwa mwongozo wa maisha yenu. Wanangu, nitawatumia, ninyi mitume wa upendo, kusaidia wanangu wote kuujua ukweli. Wanangu, mimi nimeliombea sikuzote Kanisa la Mwanangu, kwa hiyo nawasihi ninyi pia kufanya vile vile. Salini ili wachungaji wenu waangazwe kwa upendo wa Mwanangu. Nawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa, nipo hapa katikati yenu. Ninawatazama, ninawapa tabasamu na kuwapenda kama mama peke yake awezavyo kufanya. Kwa neema ya Roho Mtakatifu ajaye kwa njia ya usafi wangu, ninaona mioyo yenu na kuitolea kwa Mwanangu. Tangu muda mrefu nawaombeni muwe mitume wangu, na kusali kwa ajili ya wale wasioujua upendo wa Mungu. Naomba sala inayotokana na upendo, sala itoayo matunda na sadaka. Msipotee muda kutaka kuelewa kama mnastahili kuwa mitume wangu, Baba aliye Mbinguni atahukumu wote, lakini ninyi mpendeni na msikilizeni. Najua ya kuwa mambo hayo yote yanawafadhaisha, hata ujio wangu katikati yenu, lakini upokeeni kwa furaha na salini ili muelewe kwamba mnastahili kufanya kazi kwa ajili ya ufalme wa mbingu. Upendo wangu ni juu yenu. Salini ili upendo wangu udumu ndani ya kila moyo, kwa maana upendo huo unaosamehe ujitolea bila kukata tamaa. Nawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa, ninyi ni nguvu yangu. Ninyi, mitume wangu, ambao, kwa upendo wenu, unyenyekevu na sala ya kimya kimya, mnamwezesha Mwanangu ajulikane. Ninyi mnaishi ndani yangu. Ninyi mnanibeba mioyoni mwenu. Ninyi mnajua ya kuwa mna Mama awapendaye na aliyekuja kuwaletea upendo. Nawatazama katika Baba wa Mbinguni, natazama fikira zenu, maumivu yenu, mateso yenu na kuyaleta kwa Mwanangu. Msiogope! Msipoteze matumaini, maana Mwanangu humsikiliza Mama yake. Yeye hupenda tangu alipozaliwa, na ndio furaha yangu ya kuwa wanangu wote wajue upendo huo; na wote wale ambao, kwa sababu ya maumivu yao na kutoelewa kwao, walimwacha waweze kurudi kwake, na wote wao wasiomjua wamjue. Kwa sababu hiyo ninyi hapa ni mitume wangu, nami pia pamoja nanyi kama Mama yenu. Salini ili kuwa imara katika imani, maana upendo na rehema hutoka katika imani imara. Kwa njia ya upendo na rehema mtawasaidia wale wote wasiofahamu ya kuwa wanachagua giza badala ya nuru. Salini kwa ajili ya wachungaji wenu, maana wao ni nguvu ya Kanisa ambayo Mwanangu aliwaachieni. Kwa njia ya Mwanangu wao ni wachungaji wa roho. Nawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa, nimewachagua ninyi, mitume wangu, kwa maana kila mmoja wenu huchukua ndani yake jambo njema. Ninyi mnaweza kunisaidia ili ule upendo ambao kwao Mwanangu amekufa, na kufufuka baadaye, ushinde tena. Kwa hiyo nawaalika, mitume wangu, kujaribu kuona katika kila kiumbe cha Mungu, katika wanangu wote, kitu chema na kujitahidi kuwaelewa. Wanangu, ninyi nyote ni kaka na dada kwa njia ya huyo Roho Mtakatifu. Ninyi mliojaa upendo kwa ajili ya Mwanangu, mnaweza kuwaeleza wote ambao hawajui cho chote kuhusu upendo huo, yote mnayoyafahamu. Ninyi mmejua upendo wa Mwanangu, mnaelewa ufufuko wake, na mnamgeuzia macho kwa furaha. Haja yangu ya kimama ni kwamba wanangu wote waungane katika upendo wa Yesu. Kwa hiyo nawaalika, mitume wangu, kuishi kwa furaha Ekaristi maana, katika Ekaristi, mwanangu anajitoa kwa ajili yenu tena na tena, na kwa mfano wake, anawaonyesha namna ya kutoa upendo na sadaka kwa jirani. Nawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa, fungueni mioyo yenu mkajaribu kuhisi jinsi ninavyowapenda na kutaka mpendeni Mwanangu. Nataka mpende zaidi kwa kuwa haiwezekani kumjua pasipo kumpenda, maana Yeye ndiye upendo. Wanangu, mimi nawajueni: najua maumivu yenu na mateso yenu maana niliyaishi. Nafurahi pamoja nanyi kwa furaha zenu. Nalia machozi pamoja nanyi katika maumivu yenu. Sitawaacheni kamwe. Nitaongea nanyi daima kwa upole wa kimama na, kama mama, nahitaji mioyo yenu ifumbuliwe, ili kwa hekima na unyofu mueneze upendo wa Mwanangu. Nawahitaji ninyi mfumbuliwe na kuwa wepesi kupokea mema na huruma. Nahitaji muungano wenu na Mwanangu, kwa maana nataka mpate kufanikiwa na kumsaidia kuleta heri kwa wanangu wote. Mitume wangu, nawahitaji, ili muwaonyeshe wote ukweli wa Mungu, ili moyo wangu, ulioteswa na kuteswa hata leo kupita kiasi, uweze kushinda katika upendo. Salini kwa ajili ya utakatifu wa wachungaji wenu, ili katika jina la Mwanangu, waweze kutenda maajabu, maana utakatifu hutenda maajabu. Nawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa, nataka kufanya kazi kwa njia yenu, wanangu, mitume wangu, ili mwishowe niweze kukusanya wanangu wote pale ambapo pameandaliwa tayari kwa ajili ya furaha yenu. Nawaombea, kusudi kwa matendo yenu muweze kugeuza, kwani muda umefika kwa matendo ya kweli, kwa ajili ya Mwanangu. Upendo wangu utafanya kazi ndani mwenu, nitawatumia ninyi. Muwe na imani nami, kwani yote ninayotamani, ninayatamani kwa ajili yenu, wema wa milele, ulioumbwa kwa njia ya Baba wa Mbinguni. Ninyi, wanangu, mitume wangu, muishi maisha ya duniani pamoja na wanangu ambao hawafahamu upendo wa Mwanangu, wale ambao hawaniiti mama. Lakini msiogope kushuhudia ukweli, kwa maana ikiwa ninyi hamtaogopa na kushuhudia ukweli kwa uhodari, ukweli utashinda kimuujiza. Kumbukeni: nguvu iko katika upendo. Wanangu, upendo ndio kutubu, kusamehe, kusali, kujitoa sadaka na rehema, maana mkijua kupenda kwa matendo mtawabadilisha na wengine, mtawezesha mwanga wa Mwanangu uingie katika mioyo yao. Nawashukuru. Muwaombee wachungaji wenu, wao ni mali ya Mwanangu. Yeye aliwaita. Salini ili wawe siku zote na nguvu na uhodari wa kung'aa kwa nuru ya Mwanangu. Nawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa, nawaalika kueneza imani katika Mwanangu, imani yenu. Ninyi wanangu, mlioangazwa na Roho Mtakatifu, mitume wangu, itangazeni imani kwa watu wengine, yaani kwa wasiosadiki, wasioijua na wasiotaka kuijua. Kwa sababu hiyo yawapasa kusali sana kwa ajili ya zawadi ya upendo, maana upendo ndio alama maalum ya imani ya kweli, na ninyi mtakuwa mitume wa upendo wangu. Upendo hufanya upya daima maumivu na furaha ya Ekaristi, hufanya upya maumivu ya Mateso ya Mwanangu, aliyewaonyesha upendo usio na kifani; hufanya upya furaha ya tendo la kuwaachia Mwili wake na Damu yake kwa ajili ya kuwalisha na hivyo kuwa kitu kimoja nanyi. Nikiwaangalia kwa wema nahisi upendo pasipo kiasi, ulioniimarisha katika hamu yangu ya kuwaongoza katika imani thabiti. Imani thabiti itawapa furaha na uchangamfu duniani, na mwishowe kuwaunganisha na Mwanangu. Hiyo ndiyo hamu yake. Kwa hiyo mwishi katika Yeye, na katika upendo, isheni katika nuru iliyowaangaza daima katika Ekaristi. Nawaombeni kusali sana kwa wachungaji wenu, kusali ili kupata upendo mkubwa kwa ajili yao, kwa maana Mwanangu aliwapeni ili waweze kuwalisha kwa Mwili wake na kuwafundisha upendo. Kwa hiyo wapendeni ninyi pia! Lakini, wanangu, kumbukeni: upendo maana yake ni kuvumilia na kutoa na kutohukumu kamwe. Nawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa, mimi, kama Mama apendaye wanawe, natambua jinsi ulivyo mgumu muda huu mnaouishi. Naona mateso yenu, lakini jueni kwamba hamko peke yenu: Mwanangu yu pamoja nanyi! Yeye yupo popote, asiyeonekana, lakini mtaweza kumwona ikiwa mtamwishi. Yeye ndiye nuru inayoangaza roho yenu na kuleta amani. Yeye ndiye Kanisa, mnalopaswa kulipenda, kuliombea na kulilinda daima: si kwa maneno tu, bali kwa matendo ya upendo. Wanangu, fanyeni yote ili Mwanangu ajulikane kwa watu wote, na aweze kupendwa, kwa maana ukweli ni katika Mwanangu, aliyezaliwa na Mungu, Mwana wa Mungu. Msipoteze muda kwa kufikiri mno; mtajitenganisha na ukweli. Pokeeni Neno lake kwa moyo mnyofu na kuliishi. Mkiishi Neno lake, mtasali. Mkiishi Neno lake, mtapenda kwa upendo wenye huruma, na mtapendana. Kwa kadiri mtakavyokuwa na upendo hivyo ndivyo mtakavyokuwa mbali na kifo. Kwa wale watakaoishi na kulipenda Neno la Mwanangu, kifo kitakuwa uhai kwao. Nawashukuru! Salini kwa ajili ya kuweza kuona Mwanangu katika wachungaji wenu. Salini kwa ajili ya kuweza kumkumbatia katika wao. ”
“Wanangu wapendwa, wapendwa mitume wangu wa upendo, waletaji wangu wa ukweli, ninawaalika tena na ninawakusanya karibu nami ili mnisaidie, ili muwasaidie wanangu wote wenye kiu ya upendo na ukweli, wenye kiu ya Mwanangu. Mimi ndimi neema ya Baba wa Mbinguni iliyotumwa kuwasaidieni kuishi neno la Mwanangu. Pendaneni. Nimeyaishi maisha yenu duniani. Najua kwamba si kitu rahisi kila mara lakini, mkipendana, mtasali kwa moyo, mtafikia vilele vya maisha ya roho, na njia ya kwenda mbinguni itafunguliwa mbele yenu. Pale nawangojea mimi, Mama yenu, kwa maana mimi nipo pale. Muwe waaminifu kwa Mwanangu na muwafundishe wengine uaminifu. Mimi nipo pamoja nanyi na kuwasaidia. Nitawafundisha imani, ili muweze kuwafikishia wengine kwa njia sahihi. Nitawafundisha ukweli, ili muweze kuufahamu. Nitawafundisha upendo, ili mjue upendo wa kweli ni kitu gani. Wanangu, Mwanangu atafanya yote ili aongee kwa njia ya maneno na matendo yenu. Nawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa, nipo hapa katikati yenu kuwatieni moyo, kuwajaza kwa upendo wangu, kuwaalika tena kuwa mashahidi wa upendo wa Mwanangu. Wanangu wengi hawana tumaini, hawana amani, hawana upendo. Wao wanatafuta Mwanangu lakini hawajui jinsi wala wapi ya kumpata. Mwanangu awafungulia mikono Yake, nanyi wasaidieni ili waje mikononi Mwake. Wanangu, kwa hiyo ni lazima msali kwa upendo, lazima msali sana, sana, ili kupata upendo zaidi na zaidi, kwa maana upendo hushinda mauti na hudumisha maisha. Watume wa upendo wangu, wanangu wenye moyo mnyofu na safi, jiungeni zaidi na zaidi katika kusali. Mnatengana sana! Jipeni moyo katika kukua kiroho, kama vile Mimi ninawapeni moyo. Ninawaangalia na nipo karibu nanyi kila mnaponifikiria. Waombeeni wachungaji wenu, wale walioacha yote kwa ajili ya Mwanangu. Wapendeni na waombeeni, Baba wa Mbinguni husikiliza sala zenu. Nawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa, nataka kuongea nanyi tena juu ya upendo. Nimewakusanya kunizunguka kwa Jina la Mwanangu, kwa kadiri ya mapenzi yake. Nataka imani yenu iwe thabiti na iwe inatokana na mapendo, kwa maana wanangu wale wanaoelewa upendo wa Mwanangu na kuufuata, huishi katika mapendo na matumaini. Wamejua upendo wa Mungu. Kwa hiyo, wanangu, salini, salini ili muweze kupenda zaidi muwezavyo na kutenda matendo ya upendo. Kwa maana, imani peke yake, pasipo upendo wala matendo ya upendo, si neno ninaloomba kwenu. Wanangu, ule ni utovu wa imani, ni kujisifu mwenyewe. Mwanangu hutaka imani na matendo, upendo na wema. Mimi ninasali, lakini nawaombeni pia kusali na kuishi upendo, kwa maana nataka ya kuwa Mwanangu, atakapoona mioyo ya wanangu wote, aweze kuona ndani yake upendo na wema, sio chukio na ubaridi. Wanangu, mitume ya upendo wangu, msipoteze tumaini, msikate tamaa: ninyi mnaweza kufanya! Mimi ninawapeni moyo na kuwabariki, maana yote yaliyopo duniani hapa - ambayo kwa bahati mbaya wanangu wengi huweka mahali pa kwanza - yatatoweka na upendo na matendo ya upendo tu zitabaki, nazo zitawafungulia malango ya Ufalme wa Mbinguni. Nitawangojea karibu na malango hayo, karibu na malango hayo nataka kuwangojea na kuwakumbatia wanangu wote. Nawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa, mimi ni sikuzote pamoja nanyi, kwa maana Mwanangu alinikabidhi ninyi. Nanyi, wanangu, mnanihitaji mimi, mnitafute, mnijie na mfurahishe Moyo wangu wa kimama. Mimi ninawapenda na nitawapenda ninyi mnaoteseka na kutolea mateso yenu kwa ajili ya Mwanangu na kwa ajili yangu. Upendo wangu hutafuta upendo wa wanangu wote na wanangu wote hutafuta upendo wangu. Kwa njia ya upendo Yesu hutafuta ushirika kati ya Mbingu na dunia, kati ya Baba wa mbinguni na ninyi, wanangu, Kanisa lake. Kwa hiyo lazima kusali sana, kusali na kulipenda Kanisa ambalo ninyi ni wake. Sasa Kanisa linateseka na kuhitaji mitume ambao, wakipenda ushirika, wanaposhuhudia na kutoa, waonyeshe njia za Mungu. Kanisa linahitaji mitume ambao, wakiishi Ekaristi kwa moyo, watende matendo makuu. Kanisa linawahitaji ninyi, mitume wangu wa upendo. Wanangu, Kanisa limeteswa na kusalitiwa tangu siku zake za awali, lakini linazidi kukua siku hata siku. Kanisa halitaharibiki, kwa maana Mwanangu alilipa moyo: Ekaristi. Nuru ya ufufuo wake imeng’aa na itang’aa juu yake. Kwa hiyo msiogope! Waombeeni wachungaji wenu, ili wawe na nguvu na upendo kwa kuwa madaraja ya wokovu. Nawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa, kama Mama nafurahi ya kuwa katikati yenu, kwa maana nataka kuongea nanyi tena kuhusu maneno ya Mwanangu na upendo wake. Natumaini mtanipokea kwa upendo, maana maneno ya Mwanangu na upendo wake ni nuru na tumaini la pekee katika giza la siku hizi. Huu ni ukweli wa pekee, nanyi mtakaoupokea na kuuishi, mtakuwa na mioyo safi na minyenyekevu. Mwanangu hupenda mioyo safi na minyenyekevu. Mioyo safi na minyenyekevu inahuisha maneno ya Mwanangu: inayaishi, inayaeneza na kufanya hata wote wayasikie. Maneno ya Mwanangu yanaamsha maisha ya wale wanaoyasikiliza, maneno ya Mwanangu hurudisha upendo na matumaini. Kwa hiyo, mitume wangu wapenzi, wanangu, isheni maneno ya Mwanangu. Pendaneni kama Yeye alivyowapenda. Pendaneni katika jina lake na kumbukumbu lake. Kanisa huendelea na kukua kwa ajili ya wale wanaosikiliza maneno ya Mwanangu, kwa sababu ya wanaohuzunika na kuteseka kimyakimya katika tumaini la kukombolewa milele. Kwa hiyo wanangu wapendwa, maneno ya Mwanangu na upendo wake yawe wazo la kwanza na la mwisho la siku yenu. Nawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa, nimewaalika na ninawaalika tena kumjua Mwanangu, kuujua ukweli. Mimi nipo pamoja nanyi na ninasali ili mfanikiwe. Wanangu, yawapasa kusali sana ili kupata upendo na uvumilivu mwingi kadiri muwezavyo, ili kuweza kuvumilia sadaka na kuwa maskini rohoni. Mwanangu, kwa njia ya Roho Mtakatifu, yu sikuzote pamoja nanyi. Kanisa lake huzaliwa katika kila moyo unaomjua. Salini ili muweze kumjua Mwanangu, salini ili roho yenu iwe kitu kimoja pamoja naye. Hiyo ndiyo sala na huo ndio upendo wa kuwavutia wengine na kuwafanyeni kuwa mitume wangu. Ninawatazama kwa upendo, kwa upendo wa kimama. Ninawajua, najua maumivu yenu na mateso yenu, kwa maana Mimi nami niliteswa kimya. Imani yangu ilinipa upendo na tumaini. Ninawaambieni tena: Ufufuo wa Mwanangu na Kupokewa kwangu mbinguni ni tumaini na upendo kwa ajili yenu. Kwa hiyo, wanangu, salini ili kujua ukweli, ili kupata imani thabiti, ya kuongoza mioyo yenu na kuweza kugeuza mateso yenu na maumivu yenu kuwa upendo na tumaini. Nawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa, ujio wangu kwenu ni zawadi ya Baba wa Mbinguni kwa ajili yenu. Kwa njia ya upendo wake ninakuja kuwasaidieni kupata njia inayowangoza kwenye ukweli, na kupata njia inayowaongoza kwa Mwanangu. Ninakuja kuwathibitishia ukweli. Nataka kuwakumbushia maneno ya Mwanangu. Yeye aliyatamka maneno ya wokovu kwa ulimwengu wote, maneno ya upendo kwa watu wote, ule upendo aliouonyesha kwa kujitolea kwake sadaka. Lakini hata leo wanangu wengi hawamjui, hawataki kumjua, hawamjali. Kwa sababu ya kutokujali kwao, moyo wangu unateseka kwa uchungu. Mwanangu amekuwa daima katika Baba. Alipozaliwa duniani, ametuletea Umungu, wakati kutoka kwangu ameuchukua ubinadamu. Kwa njia yake Neno limefika katikati yetu. Kwa njia yake Mwanga, ambao hupenyeza mioyoni, huiangaza, huijaza upendo na faraja, umeingia ulimwenguni. Wanangu, wanaweza kumwona Mwanangu wale wote wanaompenda, kwa kuwa uso wake huonekana kwa njia ya mioyo inayojaa mapendo kumwelekea Yeye. Kwa hiyo, wanangu, mitume wangu, mnisikilize! Acheni uovu na ubinafsi. Msiishi tu kwa ajili ya vitu vya ulimwengu, vinavyoharibika. Mpendeni Mwanangu na muwawezeshe wengine kuutambua uso kwa njia ya mapendo mliyo nayo kwake. Mimi nitawasaidia kumjua zaidi. Mimi nitawaeleza kuhusu Yeye. Nawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa, msiwe na mioyo migumu, iliyofungwa na iliyojaa hofu. Pokeeni upendo wangu wa kimama uiangaze na kuijaza mioyo yenu upendo na matumaini, ili, kama Mama, niyalainishe maumivu yenu: ninayajua, na nimeyaonja. Maumivu huinua nayo ni sala kuu kuliko zote. Mwanangu huwapenda hasa wanaopokea maumivu. Alinituma Mimi niyalainishe na kuwaletea matumaini. Mumwamini Yeye. Najua kuwa ni vigumu kwenu, maana mnaona giza linalozidi kuongeza karibu yenu pande zote. Wanangu, giza mtalivunja kwa njia ya sala na upendo. Yule anayesali na kupenda haogopi, ana matumaini na upendo wenye huruma: Anaona mwanga, na anamwona Mwanangu. Kama mitume wangu nawaalika mjaribu kuwa mfano wa upendo wenye huruma na wenye matumaini. Salini sikuzote tena kwa ajili ya kupata upendo mwingi kadiri muwezavyo, maana upendo huleta mwanga unaovunja kila giza, na humleta Mwanangu. Msiogope, ninyi si peke yenu: Mimi nipo pamoja nanyi! Ninawasihi waombeeni wachungaji wenu, ili wawe na upendo kila wakati na wawe na matendo ya upendo kwa Mwanangu, kwa njia yake na kwa kumkumbuka Yeye. Nawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa, Moyo wangu wa kimama hutaka wongofu wenu mnyofu na ya kuwa muwe na imani thabiti, ili muweze kuwatangazia watu wote wanaowazunguka upendo na amani. Lakini, wanangu, msisahau: kila mmoja wenu mbele ya Baba aliye Mbinguni ni ulimwengu wa pekee! Kwa hiyo nguvu ya Roho Mtakatifu isiyo kifani iweze kutenda kazi ndani mwenu! Muwe wanangu safi kwa kiroho. Katika karama ya kiroho kuna uzuri. Yote yaliyo ya kiroho ni hai na nzuri ajabu. Msisahau ya kuwa katika Ekaristi, iliyo moyo wa imani, Mwanangu yu daima pamoja nanyi. Yeye anawajia na pamoja nanyi humega mkate maana, Mwanangu, kwa ajili yenu amekufa, amefufuka akaja tena. Haya maneno yangu ni ya muhimu kwa maana ni ukweli, na ukweli haubadiliki: lakini wanangu wengi hawayatambui. Wanangu, maneno yangu si mazee wala mapya, ni ya milele. Kwa hiyo nawaalika ninyi, wanangu, kuangalia alama za nyakati, na "kukusanya misalaba yaliyovunjika" na kuwa mitume wa Ufunuo. Nawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa, kama Mama wa Kanisa, kama Mama yenu, ninatabasamu nikiwaona kunijia, kukusanyika kandokando yangu na kunitafuta. Ujio wangu katikati yenu ni onyesho la kadiri Mbingu inavyowapenda. Ujio wangu unawaonyesha njia ya kuelekea kwenye uzima wa milele, kuelekea wokovu. Mitume wangu, ninyi mnaojaribu kuwa na moyo safi na Mwanangu ndani yake, ninyi mpo katika njia njema. Ninyi mnamtafuta Mwanangu, mnatafuta njia njema. Yeye aliacha dalili nyingi za upendo wake. Ameacha tumaini. Ni rahisi kumpata, ikiwa mpo tayari kujitolea na kutubu, ikiwa mtakuwa na uvumilivu, rehema na upendo kwa jirani. Wanangu wengi hawaoni wala hawasikii maana hawataki. Hawapokei maneno na matendo yangu, lakini Mwanangu, kwa njia yangu, anawaalika wote. Roho yake huangaza wote katika mwanga wa Baba wa Mbinguni, katika ushirika kati ya Mbingu na dunia, katika upendano; maana upendo huita upendo na kutenda ili matendo yawe muhimu kuliko maneno. Kwa hiyo, mitume wangu, mliombee Kanisa lenu, lipende na tendeni matendo ya upendo. Ingawa limesalitiwa na kujeruhiwa, lipo hapa kwa sababu hutoka kwa Baba wa Mbinguni. Muwaombeeni wachungaji wenu, ili kuona ndani yao ukuu wa upendo wa Mwanangu. Nawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa, uwepo wangu halisi na wa uhai katikati yenu uwafanye kuwa wenye furaha kwani huo ni upendo mkuu wa Mwanangu. Yeye ananituma katikati yenu ili, kwa upendo wa kimama, Mimi niwaimarishe; ili muelewe kwamba maumivu na furaha, mateso na mapendo husaidia nafsi yenu kuishi kwa bidii zaidi; ili niwaalike tena kuadhimisha Moyo wa Yesu, moyo wa imani: Ekaristi. Mwanangu, siku kwa siku, hurudi hai katikati yenu: huwarudia, hata kama hakuwaacha kamwe. Wakati mmoja wenu, wanangu, anamrudia, Moyo wangu wa kimama hushtuka kwa furaha. Kwa hiyo Wanangu, irudieni Ekaristi, mrudieni Mwanangu. Njia ya kumrudia Mwanangu ni ngumu na imejaa kujinyima lakini mwishowe, kuna mwanga siku zote. Naelewa maumivu yenu na mateso yenu, na kwa upendo wa kimama, ninapangusa machozi yenu. Mtumainini Mwanangu, kwa maana Yeye atawafanyieni neno msilojua hata kuomba. Ninyi, wanangu, fikirieni nafsi yenu tu, kwani nafsi ni kitu cha pekee mliyo nayo duniani. Chafu ama safi, mtaichukua mbele ya Baba aliye Mbinguni. Kumbukeni: imani katika upendo wa Mwanangu hulipwa siku zote. Nawaambieni kuwaombea hasa wale ambao Mwanangu aliwaita kuishi wakimfuata na kulipenda kundi lao. Nawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa, nimekuja kwenu, katikati yenu, ili mnipe mahangaiko yenu, niweze kuyaleta mbele ya Mwanangu na kuwaombeeni kwake kwa manufaa yenu. Najua kuwa kila mmoja wenu ana mahangaiko yake, majaribu yake. Kwa hiyo kwa moyo wa kimama nawaalikeni: Njooni kwenye Meza ya Mwanangu! Yeye humega mkate kwa ajili yenu, huwapa Yeye mwenyewe. Huwapa matumaini. Anawaomba kuwa na imani zaidi, matumaini zaidi, utulivu zaidi. Anawaomba mpigane ndani yenu dhidi ya ubinafsi, hukumu na udhaifu wa kibinadamu. Kwa hiyo Mimi, kama Mama, nawaambieni: salini, maana sala huwapa nguvu ya kupigana ndani yenu. Mwanangu, alipokuwa mtoto, aliniambia mara nyingi ya kuwa wengi watanipenda na kuniita "Mama". Mimi hapa, katikati yenu, nasikia upendo na kuwashukuru! Kwa njia ya upendo huu namwomba Mwanangu ili hakuna hata mmoja wenu, wanangu, arudiye nyumbani jinsi alivyokuja. Ili mlete matumaini, rehema na upendo kadiri muwezavyo; ili muwe mitume wa upendo wangu, wanaoshuhudia kwa maisha yao kwamba Baba aliye Mbinguni ni chemchemi ya uzima si ya mauti. Wanangu wapendwa, nawaomba tena kwa moyo wa kimama: waombeeni wateule wa Mwanangu, kwa ajili ya mikono yao iliyobarikiwa, kwa ajili ya wachungaji wenu, ili waweze kumhubiri Mwanangu kwa upendo mwingi wawezavyo, na hivyo kusababisha wongofu. Nawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa, kulingana na mapenzi ya Mwanangu na upendo wangu wa kimama naja kwenu, wanangu, hasa kwa wale ambao hawajajua bado upendo wa Mwanangu. Ninakuja kwenu mnaonifikiria, mnaoomba msaada wangu. Ninawapa upendo wangu wa kimama na kuwaletea baraka ya Mwanangu. Mnayo mioyo safi na wazi? Mnaona dalili za uwepo wangu na upendo wangu? Wanangu, katika maisha yenu ya dunia igieni moyo na mfano wangu. Maisha yangu yalikuwa maumivu, ukimya, imani na matumaini pasipo mipaka katika Baba wa Mbinguni. Hakuna kitu cha bahati: si maumivu, si furaha, si mateso, si upendo. Hizo zote ni neema ambazo Mwanangu anawapeni na zinazowaongoza kwenye uzima wa milele. Mwanangu anawaomba mapendo na sala ndani yake. Kupenda na kusali ndani yake maana yake — kama Mama nataka kuwafundisha — ni kusali katika ukimya wa nafsi zenu, si kusema kwa midomo tu. Ni tendo dogo zuri litendwalo kwa jina la Mwanangu; ni uvumilivu, rehema, upokeaji wa maumivu na kujitolea kwa ajili ya wengine. Wanangu, Mwanangu huwatazama. Ombeni ili ninyi pia muuone uso wake, na ili uso huo uweze kufunuliwa kwenu. Wanangu, mimi nawafunulia ukweli halisi wa pekee. Salini kwa kuyaelewa na kuweza kueneza mapendo na matumaini, kwa kuweza kuwa mitume wa upendo wangu. Moyo wangu wa kimama hupenda hasa wachungaji. Iombeeni mikono yao iliyobarikiwa. Nawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa, Roho Mtakatifu, kwa njia ya Baba wa Mbinguni, amenifanya Mama: Mama wa Yesu na, kwa hiyo, Mama yenu vilivile. Kwa hiyo nawajilia niwasikilize, niwafungulie mikono yangu ya kimama, niwapeni Moyo wangu na kuwaalika kukaa pamoja nami, kwa maana kutoka juu ya msalaba Mwanangu amenikabidhi ninyi. Kwa bahati mbaya wanangu wengi hawakujua upendo wa Mwanangu, wengi hawataka kumjua. Loo, wanangu, mabaya mengi yatoka kwa wale ambao hawana budi ya kuona na kuelewa ili kuamini! Kwa hiyo, wanangu, mitume wangu, katika kimya ya moyo wenu sikilizeni sauti ya Mwanangu, ili moyo wenu uwe makazi yake wala usiwe giza na huzuni, bali uangaziwe na mwanga wa Mwanangu. Tafuteni matumaini kwa imani, maana imani ni maisha ya roho. Ninawaalika tena: salini! Salini ili kuishi imani katika unyenyekevu, katika amani ya kiroho na mkiangaziwa na mwanga. Wanangu, msijaribu kuelewa yote mara moja, maana Mimi nami sikuelewa yote mara moja, lakini niliyaamini maneno ya kimungu aliyoyasema Mwanangu, Yeye aliyekuwa mwanga wa kwanza na mwanzo wa Ukombozi. Enyi mitume wa moyo wangu, ninyi mnaosali, mnaojitolea, mnaopenda wala msiohukumu: ninyi nendeni mkaeneze ukweli, maneno ya Mwanangu, Injili. Ninyi kweli, ni Injili iliyo hai, ninyi ni miali ya mwanga wa Mwanangu. Mwanangu na mimi tutakuwa karibu nanyi, tutawatia moyo na kuwajaribu. Wanangu, ombeeni daima na hasa baraka ya wale ambao Mwanangu amebariki mikono yao, yaani Wachungaji wenu. Nawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa, kuja na kujifunua kwangu kwenu ni furaha kubwa ya Moyo wangu wa kimama. Ni zawadi ya Mwanangu kwa ajili yenu na ya wale watakaokuja. Kama Mama nawaalika: mpendeni Mwanangu kuliko yote! Ili kumpenda kwa moyo wote, yawapaswa kumjua: Mtamjua kwa kusali: Salini kwa moyo na hisia zenu. Kusali maana yake ni kutafakari upendo wake na kujitolea kwake. Kusali maana yake ni kupenda, kutoa, kuteseka na kutolea sadaka. Nawaalika ninyi, wanangu, kuwa mitume ya sala na upendo. Wanangu, ni wakati wa kukesha. Katika kesha hii nawaalika kusali, kupenda na kutumaini. Maadamu Mwanangu ataangalia mioyo yenu, Moyo wangu wa kimama unatamani kwamba Yeye aone ndani ya mioyo yenu tumaini timilifu na upendo. Upendo wa mitume wangu wote pamoja utaishi, utashinda na utafunua maovu. Wanangu, mimi nilikuwa kalisi ya Mtu - Mungu, nilikuwa chombo cha Mungu. Kwa hiyo nawaalika ninyi, mitume wangu, kuwa kalisi ya upendo mnyofu na safi wa Mwanangu. Nawalika kuwa chombo ambacho kwa njia yake wote wasiojua upendo wa Mungu, wasiopenda kamwe, wataelewa, wataupokea na wakaokolewa. Nawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa, Moyo wangu wa kimama unalia machozi ninapoyaona yale wanayoyafanya wanangu. Dhambi zinaongezeka, usafi wa moyo unaendelea kupoteza umuhimu wake. Mwanangu amesahauliwa na upendo kwake unaendelea kupunguka na wanangu wanateswa. Kwa hiyo, wanangu, mitume wa moyo wangu, iteni jina la Mwanangu kwa nafsi na kwa moyo: Yeye atakuwa na maneno ya mwanga kwenu. Naye atajionyesha kwenu, anashiriki Mkate pamoja nanyi na anawapa maneno ya upendo, ili myageuze kuwa matendo ya huruma na muwe hivyo mashahidi ya ukweli. Kwa hiyo, wanangu, msiogope! Acheni Mwanangu awe ndani yenu. Yeye atawatumia ninyi ili kuzitibu nafsi zinazojeruhiwa na kuziongoka zile zinazopotea. Kwa hiyo, wanangu, rudieni kusali Rozari. Mwisali kwa roho ya ukarimu, ya sadaka na ya huruma. Salini si kwa maneno tu, ila kwa matendo ya huruma. Salini kwa upendo kwa watu wote. Mwanangu amekuza kimaadili upendo kwa njia ya sadaka yake. Kwa hiyo isheni pamoja naye mpate nguvu na matumaini, mpate upendo ulio uhai wa kuongoza kwenye uzima wa milele. Kwa njia ya upendo wa Mungu mimi nami ni pamoja nanyi, na nitawaongoza kwa upendo wa kimama. Nawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa, Mwanangu alikuwa chemchemi ya upendo na mwanga alipoongea na watu wa mataifa yote. Mitume wangu, fuateni mwanga wake, si rahisi, yawapasa kuwa wadogo, yawapasa kuwa wadogo kuliko wengine wote na kwa msaada wa imani kujazwa na upendo wake. Hakuna mtu duniani, pasipo imani, awezaye kuwa na uzoefu wa mwujiza. Mimi nipo pamoja nanyi, ninajionyesha kwa matokeo hayo, kwa maneno hayo, nataka kuwashuhudia upendo wangu na utunzaji wangu wa kimama. Wanangu, msipoteze wakati mkiweka maswali ambayo hamtapata kamwe majibu, maisha yenu duniani yatakapomalizika Baba wa Mbinguni atawajibu. Mjue daima ya kuwa Mungu hujua yote, Mungu huona, Mungu hupenda. Mwanangu mpenzi sana huangaza maisha na kupasua giza. Upendo wa kimama unaonileta kwenu hauelezeki, umefichwa lakini ni halisi, ninawaonyesheni hisia zangu, upendo, hisani na ukarimu wangu wa kimama. Kutoka kwenu, mitume wangu, ninatafuta sala zenu: mawaridi yaliyo matendo ya upendo, hizo ndizo kwa moyo wangu wa kimama sala za kunipendeza sana, haya ninayaletea Mwanangu aliyezaliwa kwa ajili yenu. Yeye anawatazama ninyi na kuwasikia. Sisi tupo kila siku karibu nanyi kwa upendo wenu ambao huita, huunga, huongoa, hutia moyo na kujaza. Kwa hiyo mitume wangu pendaneni daima, lakini hasa mpende Mwanangu, hii ni njia ya pekee ya wokovu kuelekea uzima wa milele, hiyo ni sala ya kunipendeza ambayo kama harufu nzuri ajabu ya mawaridi, hujaa moyo wangu. Ombeni daima, waombeeni wachungaji wenu ili wapate nguvu ya kuwa mwanga wa Mwanangu. Nawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa, ninyi mnaojaribu kumtolea Mwanangu kila siku ya maisha yenu, ninyi mnaojaribu kuishi pamoja naye, ninyi mnaosali na kujitolea, ninyi ni matumaini katika ulimwengu huu wenye udhia. Ninyi ni miali ya mwanga wa Mwanangu, Injili iliyo hai, na ninyi ni mitume wangu wapenzi wa upendo. Mwanangu ni pamoja nanyi. Vili vile, lakini, Yeye anawangojea kwa uvumilivu wale wasiomjua. Kwa hiyo ninyi, mitume wa upendo wangu, salini kwa moyo na onyesheni kwa matendo upendo wa Mwanangu. Kwenu ninyi hiyo ni matumaini ya pekee, na njia ya pekee kuelekea uzima wa milele. Mimi, kama Mama, ni hapa pamoja nanyi. Sala zenu mnazoniomba ni kwangu mawaridi ya upendo mazuri kuliko yote, Siwezi kutokuwapo pale ninapohisi harufu ya mawaridi. Kuna matumaini! Nawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa, kwa upendo wa kimama naja kuwasaidieni kuwa na upendo zaidi, maana yake imani zaidi. Naja kuwasaidieni kuishi kwa upendo maneno ya Mwanangu, ili ulimwengu uwe tofauti. Kwa sababu hiyo nawakusanya, mitume wa mapendo yangu, karibu nami. Niangalieni kwa upendo, ongeeni nami kama vile na Mama kuhusu mateso yenu, maumivu yenu, furaha zenu. Ombeni ili nisali Mwanangu kwa ajili yenu. Mwanangu ni mwenye rehema na haki. Moyo wangu wa kimama ungependa ninyi pia muwe hivyo. Moyo wangu wa kimama ungependa ya kuwa ninyi, mitume wa mapendo yangu, mngeongea kwa maisha yetu juu ya Mwanangu na juu yangu pamoja na watu wote walio karibu nanyi, ili ulimwengu uwe tofauti, ili wairudie imani na tumaini. Kwa hiyo, wanangu, salini, salini, salini kwa moyo. Salini kwa upendo, salini kwa matendo mema. Salini ili wote wamjue Mwanangu, ili ulimwengu ugeuke, ulimwengu uokoke. Ishini kwa upendo maneno ya Mwanangu. Msihukumu, lakini mpendaneni, ili Moyo wangu uweze kushinda. Nawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa, mitume wa upendo wangu, inawapasa ninyi kuujulisha upendo wa Mwanangu kwa wale wote ambao hawakumjua. Inawapasa ninyi, mianga midogo ya ulimwengu, ambao mimi ninaifunza kwa upendo wa kimama ili ing'ae waziwazi kwa mwangaza kamili. Sala itawasaidia, maana sala huwaokoa ninyi, sala huuokoa ulimwengu. Kwa hiyo, wanangu, salini kwa maneno, kwa moyo, kwa upendo wenye huruma na kwa sadaka. Mwanangu aliwaonyesha njia: Yeye aliyejimwilisha na kunifanya kuwa kalisi ya kwanza; Yeye ambaye kwa sadaka yake isiyo na kifani aliwaonyesha kama inavyopaswa kupenda. Kwa hiyo, wanangu, msiogope kusema kweli. Msiogope kujigeuza wenyewe na ulimwengu ili kueneza mapendo, mkitenda kila jinsi kusudi Mwanangu aweze kujulikana na kupendwa kwa kuwapenda wengine kwa ajili yake. Mimi, kama mama, nipo daima pamoja nanyi. Namwomba Mwanangu awasaidie ili katika maisha yenu upendo utawale: upendo uishio, upendo uvutao, upendo utoao uzima. Huo ndio upendo ninaowafundisha, upendo safi. Inawapasa ninyi, mitume wangu, kuutambua, kuuishi, kuueneza. Waombeeni wachungaji wenu kwa moyo, ili waweze kumshuhudia Mwanangu kwa upendo. Nawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa, nawaalika kusali pasipo kuomba, bali mkitoa sadaka, mkijitolea wenyewe. Nawaalika kuleta habari ya ukweli na upendo wenye rehema. Ninamwomba Mwanangu kwa ajili yenu, kwa imani yenu, inayoendelea kupunguka katika mioyo yenu. Ninamwomba awasaidieni kwa Roho ya Mungu, kama vile mimi nami ninavyotaka kuwasaidieni kwa roho ya kimama. Wanangu, itawabidi kujiboresha! Wale tu walio safi, wanyenyekevu na wamliojaa upendo wanautegemeza ulimwengu, wanaokoa ulimwengu na wao wenyewe. Wanangu, Mwanangu ndiye moyo wa ulimwengu: lazima kumpenda na kumwomba, na si kumsaliti daima tena. Kwa hiyo ninyi, mitume wa upendo wangu, mstawishe imani katika mioyo ya watu kwa mfano wenu, kwa sala yenu na kwa upendo wenye rehema. Mimi nipo karibu nanyi na nitawasaidia. Salini ili wachungaji wenu wapate mwanga zaidi kadiri wawezavyo, ili waweze kuangaza wale wote wanaoishi gizani. Nawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa, kama vile katika mahali pengine nilipokuja, vivyo hivyo hapa pia nawaalika kusali. Salini kwa ajili ya wale wasiomjua Mwanangu, kwa ajili ya wale ambao hawajaujua upendo wa Mungu, dhidi ya dhambi, kwa ajili ya waliowekwa wakfu, kwa ajili ya wale ambao Mwanangu aliwaita ili wawe na upendo na roho yenye nguvu, kwa ajili yenu na kwa ajili ya Kanisa. Mwombeni Mwanangu, na upendo mnaohisi kwa ajili ya ukaribu, utawapa nguvu na utawatayarisha kwa matendo mema mtakayofanya kwa Jina lake. Wanangu muwe tayari. Wakati huu ni njia panda ya maisha. Kwa hiyo nawaalika tena kwa imani na matumaini, ninawaonyesha njia ya kushika. Hayo ni maneno ya Injili: Mitume wangu, ulimwengu unahitaji sana mikono yenu iliyoinuliwa mbinguni, kuelekea kwa Mwanangu na kwa Baba wa mbinguni. Ni lazima kuwa na unyenyekevu mwingi na usafi wa moyo. Mumwamini Mwanangu na jueni ya kuwa mnaweza kuwa bora zaidi daima. Moyo wangu wa kimama unatamani kwamba ninyi, mitume wa upendo wangu, muwe sikuzote mianga midogo ya ulimwengu. Mtie nuru pale giza inapotaka kutawala na kwa sala yenu na upendo wenu, muonyeshe sikuzote njia ya kweli, ziokoeni nafsi. Mimi nipo pamoja nanyi. Nawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa, nawashukuru kwa kuitikia miito yangu na kukusanyika karibu nami, Mama yenu wa mbinguni. Najua kwamba mnanifikiri kwa upendo na matumaini. Mimi ninawapendeni nyote kama vile anavyowapendeni Mwanangu ambaye, kwa upendo wake wenye huruma, ananituma nije kwenu, mara nyingi pia. Yeye, aliyekuwa mtu na aliye Mungu, Mmoja na Utatu; Yeye aliyeteswa kwa ajili yenu mwilini na nafsini. Yeye aliyejifanya Mkate ailishe nafsi zenu na hivyo kuziokoa. Wanangu, nawafundisha jinsi ya kustahili upendo wake, kumwelekeza mawazo yenu, kumwishi Mwanangu. Mitume wa upendo wangu, ninawafunika kwa joho langu kwa sababu, kama Mama yenu, nataka kuwalinda. Nawasihi: mwuombee ulimwengu wote: moyo wangu unateswa. Dhambi zinaongezeka, ni nyingi mno. Lakini kwa msaada wenu – mlio wanyenyekevu, wanyofu, wenye upendo, watawa na watakatifu – moyo wangu utashinda. Mpendeni Mwanangu kupita wote na ulimwengu wote kwa njia yake. Msisahau kabisa ya kuwa kila ndugu yenu ana ndani yake kitu cha thamani: nafsi. Kwa hiyo, wanangu, pendeni wale wote wasiomjua Mwanangu ili kwa njia ya maombi na upendo utokao katika maombi, wawe wema zaidi. Ili wema uweze kushinda ndani yao. Ili nafsi zao ziweze kuokoka na kupata uzima wa milele. Enyi mitume wangu, wanangu. Mwanangu aliwaambieni mpendane. Hiyo iandikwe mioyoni mwenu na kwa kusali jaribuni kuishi upendo huu. Nawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa, kwa mapenzi ya Baba wa mbinguni, kama Mama wa Yule anayewapendeni, nipo hapa pamoja nanyi niwasaidieni kumjua, kumfuata. Mwanangu amewaachieni nyayo za hatua zake, ili iwe rahisi zaidi kwenu kumfuata. Msiogope, msiwe na wasiwasi. Mimi nipo pamoja nanyi! Msichoke, maana sala nyingi na sadaka zinahitajiwa kuwasaidia wale wasiomwomba, wasiompenda na wasiomjua Mwanangu. Muwasaidie mkiona ndani yao ndugu zenu. Enyi mitume wa upendo wangu, sikilizeni sauti yangu ndani yenu, hisieni upendo wangu. Kwa hiyo salini: salini mkitenda, salini mkitoa. Salini kwa upendo, salini kwa matendo na kwa fikira, kwa jina la Mwanangu. Kadiri mtakavyotoa upendo, ndivyo mtakavyoupokea. Upendo utokao katika Upendo huangaza ulimwengu. Ukombozi ni upendo, na upendo hauna mwisho. Wakati Mwanangu atakapokuja tena duniani, atatafuta upendo katika mioyo yenu. Wanangu, Yeye alifanya kwa ajili yenu matendo mengi ya upendo. Ninawafundisha kuyaona, kuyaelewa na kumshukuru mkimpenda na kumsamehe sikuzote na tena jirani yako. Kwa kuwa kumpenda Mwanangu maana yake ni kusamehe. Mwanangu hapendwi, ikiwa hatuwezi kumsamehe jirani yetu, ikiwa hatuwezi kumwelewa jirani yetu, ikiwa tunamhukumu. Wanangu, faida gani kusali, msipopenda wala msiposamehe? Nawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa, nani angeweza kusema nanyi vizuri zaidi kuliko Mimi kuhusu upendo na maumivu ya mwanangu? Niliishi pamoja naye, niliteseka pamoja naye. Nikiishi maisha ya kidunia, nilionja maumivu, maana nilikuwa mama. Mwanangu alipenda michakato na kazi ya Baba wa Mbinguni, Mungu wa kweli; na, kama alivyoniambia, alikuja kusudi awakomboe ninyi. Mimi nilificha maumivu yangu kwa njia ya upendo. Bali ninyi, wanangu, ninyi mnaweka maswali mengi, hamwelewi maumivu, hamwelewi kwamba, kwa njia ya upendo wa Mungu, mnapaswa kupokea maumivu na kuyachukua. Kila mwanadamu, iwe kwa kiwango kikubwa au kidogo, yampasa afanye mang'amuzi. Lakini, tukiwa na amani rohoni na tukiwa na hali ya neema, tumaini moja lipo: ni Mwanangu, Mungu aliyezaliwa na Mungu. Maneno yake ni mbegu ya uzima wa milele: Yanapopandwa katika roho njema, huleta matunda mengi. Mwanangu amechukua maumivu maana amepokea juu yake dhambi zenu. Kwa hiyo ninyi, wanangu, mitume wa upendo wangu, ninyi mnaoteswa: mjue kwamba maumivu yenu yatakuwa mwanga na utukufu. Wanangu, wakati mnapovumilia maumivu, wakati mnapoteswa, Mbingu huingia ndani yenu, nanyi mnawapa watu wote karibu nanyi Mbingu kidogo na matumaini mengi. Nawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa, ninaongea nanyi kama Mama, kwa maneno rahisi, lakini yamejaa wingi wa upendo na wa bidii kwa wanangu, ambao kwa njia ya Mwanangu wamekabidhiwa kwangu. Mwanangu, ambaye anakuja kutoka umilele na hata sasa, anaongea nanyi kwa maneno ya uzima na anapanda upendo katika mioyo wazi. Kwa hiyo nawaomba, mitume wa upendo wangu: muwe na mioyo iliyo wazi sikuzote kurehemu na kusamehe. Wasameheni sikuzote wenzenu kama Mwanangu, kwa vile hivyo amani itakuwa ndani yenu. Wanangu, lindeni nafsi yenu, maana hiyo ndiyo ukweli wa pekee ulio wenu bila shaka. Mmeanza kusahau umuhimu wa familia. Familia haipaswi kuwa mahali pa mateso na maumivu, bali mahali pa uelewano na huruma. Familia wanaojaribu kuishi kama apendavyo Mwanangu, wanaishi wakipendana. Tangu alipokuwa angali mtoto, Mwanangu aliniambia ya kuwa watu wote kwake ni ndugu zake. Kwa hiyo kumbukeni, enyi mitume wa upendo wangu, watu wote mnaowaona ni kwenu familia yenu, ndugu kama apendavyo Mwanangu. Wanangu, msipoteze muda kufikiria na kuhangaikia mambo yajayo. Kitu chenu kimoja cha kuhangaikia kwenu kiwe vipi kuishi vema kila dakika kadiri ya Mwanangu, na tazama hiyo ndiyo ni amani! Wanangu, msisahau kabisa kuwaombea wachungaji wenu. Salini ili waweze kupokea watu wote kama wanao, ili, kama apendavyo Mwanangu, wawe kwao kama baba za kiroho. Nawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa, nikiwatazama hapa mmekusanyika kunizunguka, Mama yenu, ninaona nafsi safi nyingi. Ninawaona wanangu wengi wanaotafuta upendo na faraja lakini hakuna mtu anayewapa. Ninawaona hata wale wanaotenda mabaya maana hawana mifano myema, maana hawajamjua mwanangu. Mwanangu anawatuma ninyi kwangu, Mama, sawa kwa wote, niwafundisheni kupenda, ili muelewe ya kuwa ninyi ni ndugu. Ninatamani kuwasaidia. Mitume wa upendo wangu, kwa mwanangu yamtosha tamaa hai ya imani na upendo na atayakubali, lakini mnapaswa kustahili, kuwa na tamaa na mioyo wazi, Mwanangu huingia katika mioyo wazi. Mimi kama Mama ninatamani kwamba mjue Mwanangu katika kweli: Mungu aliyezaliwa na Mungu, kwamba mjue ukuu wa Upendo wake, ambao mnahitaji. Yeye amezichukua juu yake dhambi zenu, ameupata Ukombozi wenu, na badala yake anaomba mpendane ninyi kwa ninyi. Mwanangu ni upendo, Yeye anawapenda watu wote bila tofauti, watu wote wa nchi zote, wa mataifa yote. Ikiwa ninyi, wanangu, mngeishi upendo wa Mwanangu, ufalme wake ungekwisha kuwa duniani. Kwa hiyo, Mitume wa upendo wangu, salini, salini ili Mwanangu na upendo wake wawe ndani yenu nanyi muweze kuwa mfano wa upendo na muweze kuwasaidia wote wale ambao hawajamjua Mwanangu. Msisahau kamwe kwamba Mwanangu, mmoja na utatu, anawapendeni. Pendeni na wombeeni wachungaji wenu. Nawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa, ninawaelekea ninyi kama Mama yenu, Mama wa wenye haki, Mama wa wale wanaopenda na kuteseka, Mama wa watakatifu. Wanangu, ninyi pia mnaweza kuwa watakatifu: ni juu yenu. Watakatifu ni wale wanaompenda Baba wa Mbinguni kupita kiasi, wale wanaompenda kupita chochote. Kwa hivyo, wanangu, jaribuni daima kuboreka. Kama ninyi mnajaribu kuwa wema, mtaweza kuwa watakatifu, hata kama hamfikiri hiyo juu yenu. Kama mnafikiri kuwa wema, ninyi sio wanyenyekevu na kiburi huwatenga kutoka utakatifu. Katika ulimwengu huu wa wasiwasi, umejaa vitisho, mikono yako, mitume wa upendo wangu, inapaswa kuwa imenyoshwa katika maombi na rehema. Kwangu, wanangu, nipeni zawadi ya Rozari, mawaridi ninayopenda sana! Mawaridi yangu ni maombi yenu msemayo kwa moyo wote, na sio yale msemayo kwa midomo yenu tu. Mawaridi yangu ni matendo yenu ya maombi, imani na upendo. Wakati alipokuwa mtoto, mwanangu aliniambia kwamba watoto wangu watakuwa wengi na wataniletea mawaridi mengi. Sikuelewa, sasa najua kwamba ninyi ni watoto wale, wanaoniletea mawaridi wakati mnapompenda mwanangu kupita yote, wakati mnaposali kwa moyo wote, wakati mnapowasaidia walio maskini zaidi. Hayo ndiyo mawaridi yangu! Hii ndiyo imani, inayosababisha kila kitu katika maisha kifanyike kwa upendo; na kiburi hakijulikani; na muwe tayari daima, kusamehe upesi, bila kuhukumu na daima mjaribu kuelewa ndugu yako. Kwa hiyo, mitume wa upendo wangu, muwaombeeni wale wasiojua kupenda, wale wasiowapenda, wale waliowatenda mabaya, wale ambao hawakujua upendo wa Mwanangu. Wanangu, ninawaomba haya, kwa sababu kumbukeni: kuomba maana yake ni kupenda na kusamehe. Nawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa, wakati duniani upendo unapopunguka, wakati njia ya wokovu haipatikani, Mimi, Mama yenu, naja kuwasaidieni kujua imani ya kweli, iliyo hai na ya kina, na kuwasaidieni kupenda kabisa. Kama Mama ninatamani mpendane, muwe wema na safi. Ni hamu yangu muwe wenye haki na mpendane. Wanangu, muwe wafurahivu rohoni, muwe safi, muwe watoto. Mwanangu alisema kwamba anapenda kukaa kati ya wenye mioyo safi, maana wenye mioyo safi ni daima vijana na wafurahivu. Mwanangu aliwaambieni msameheane na mpendane. Najua kwamba si rahisi sikuzote. Mateso husababisha kukua rohoni. Ili kukua rohoni kadiri iwezekanavyo, lazima msamehe na kupenda kwa dhati na kwa kweli. Wana wangu wengi duniani hawamjui Mwanangu, hawampendi. Lakini ninyi mnaompenda Mwanangu na kumchukua moyoni salini, salini, na mkisali mumhisi Mwanangu karibu yenu. Nafsi yenu ipumue Roho yake! Mimi nipo kati yenu na kuongea juu ya mambo madogo na makubwa. Sitachoka kuwasimulieni habari ya Mwanangu, aliye upendo wa kweli. Kwa hiyo, wanangu, nifungulieni mioyo yenu, acheni niwaongoze kama mama. Muwe mitume wa upendo wa Mwanangu na wangu. Kama Mama nawasihi: msisahau wale walioitwa na Mwanangu wawaongoze. Wachukueni moyoni na muwaombee. Nawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa, ninyi ambao Mwanangu anawapenda, ninyi ambao mimi ninawapenda, msiruhusu ubinafsi, kujipenda wenyewe, zitawale duniani. Msiache upendo na wema zifichwe. Ninyi mnaopendwa, mliojua upendo wa Mwanangu, kumbukeni ya kuwa kupendwa maana yake ni kupenda. Wanangu, muwe na imani! Mnapokuwa na imani mnafurahi na mkaeneza amani, nafsi yenu inaruka kwa shangwe: katika nafsi ile yumo Mwanangu. Mnapojitolea wenyewe kwa ajili ya imani, mnapojitolea wenyewe kwa ajili ya upendo, mnapowafanyia watu wengine mema, Mwanangu hutabasamu katika nafsi yenu. Mitume wa upendo wangu, mimi, kama Mama, ninawaelekea, ninawakusanya kunizunguka na ninataka kuwaongozeni katika njia ya upendo na imani, katika njia ya kufika kwenye Nuru ya ulimwengu. Nipo hapa kwa upendo na kwa imani, kwa maana, kwa baraka yangu ya kimama, nataka kuwapeni matumaini na nguvu katika mwendo wenu, kwa sababu njia ya kuongoza kwa Mwanangu si rahisi: imejaa matendo ya kujinyima, ya kujitolea, ya kujidhabihu, ya kusamehe na ya upendo, upendo mwingi. Njia ile, lakini, hupata amani na furaha. Wanangu, msisadiki sauti za uongo zinazosemesha kwa maneno yasiyo na ukweli, mwanga usio wa ukweli. Ninyi wanangu rudini kwa Maandiko! Ninawaangalieni kwa upendo kupita kiasi na, kwa neema ya Mungu, ninajidhihirisha kwenu. Wanangu, njoni pamoja nami, nafsi yenu iruke kwa shangwe! Nawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa, Baba wa Mbinguni amenifanyia makuu, jinsi anavyowafanyia wale wote wanaompenda sana na kwa wema na uaminifu na wanaomtumikia kwa ibada. Wanangu, Baba wa Mbinguni anawapenda na kwa ajili ya upendo wake mimi nipo hapa pamoja nanyi. Ninasema nanyi: kwa nini hamtaki kuona ishara? Pamoja naye yote ni rahisi zaidi: hata mateso, tunayoishi pamoja naye, ni mepesi zaidi, maana kuna imani. Imani husaidia mateso, na maumivu pasipo imani huongoza katika kukata tamaa. Mateso tunayoyaishi na kuyatolea kwa Mungu, huinua mtu. Je, Mwanangu hakuukomboa ulimwengu kwa njia ya mateso yake makali? Mimi, kama mama yake, katika maumivu na mateso nilikaa pamoja naye, kama vile ninavyokaa pamoja nanyi. Wanangu, mimi nipo pamoja nanyi katika maisha: katika maumivu na mateso, katika furaha na upendo. Kwa hiyo muwe na matumaini: matumaini ndiyo yanayotuwezesha kuelewa ya kuwa hapa, kwenye mateso, ni uhai. Wanangu, mimi nasema nanyi; sauti yangu inasema na nafsi yenu, Moyo wangu unasema na moyo wenu: Enyi, mitume wa upendo wangu, Moyo wangu wa kimama jinsi gani unavyowapenda. Mambo haya nataka kuwafundisha. Jinsi gani Moyo wangu unataka muwe wakamilifu, lakini mtakuwa hivyo tu wakati nafsi, mwili na upendo yatakapoungana ndani yenu. Kama wanangu nawaombeni: salini sana kwa ajili ya Kanisa na kwa wahudumu wake, kwa wachungaji wenu, ili Kanisa liwe kama Mwanangu anavyolitaka: safi kama maji ya chemchemi na limejaa upendo. Nawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa, kwa njia ya upendo mkubwa wa Baba wa Mbinguni, mimi ni pamoja nanyi kama Mama yenu nanyi ni pamoja nami kama wanangu, kama mitume wa upendo wangu ambao ninakusanya daima karibu nami. Wanangu, ninyi ni wale ambao, mkisali, yawapasa kujitolea kabisa kwa Mwanangu, ili kwamba si ninyi tena mnaoishi, bali ni Mwanangu ndani yenu; ili wale wote wasiomjua wamwone ndani yenu na watake kumjua. Salini ili waone ndani yenu unyenyekevu thabiti na wema, utayari kuwatumikia wengine; waone kwamba mnaishi kwa moyo wito wenu duniani, mkishirikiana na Mwanangu. Waone ndani yenu upole, rehema na upendo kuelekea Mwanangu, kama vile kuelekea ndugu na dada zenu. Enyi mitume wa upendo wangu, hamna budi kusali sana na kutakasa mioyo yenu, ili ninyi muwe wale wa kwanza waendao katika njia ya Mwanangu; ili ninyi muwe wale wenye haki wanaoungana na haki ya Mwanangu. Wanangu, kama mitume wangu lazima muungane na ushirika utokao katika Mwanangu, ili wanangu wasiomjua Mwanangu watambue ushirika wa upendo na watake kutembea katika njia ya uzima, njia ya umoja na Mwanangu. Nawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa, Mwanangu, aliye mwanga wa upendo, yote aliyoyafanya na anayoyafanya hufanya kwa ajili ya upendo. Vivyo hivyo nanyi, wanangu, mnapoishi katika upendo, mnapompenda jirani yenu na mnapofanya mapenzi yake. Enyi mitume wa upendo wangu, jifanyeni wadogo! Mfungulieni Mwanangu mioyo yenu safi, ili Yeye aweze kutenda kazi kwa njia yenu. Kwa msaada wa imani, mjijazie upendo. Lakini, wanangu, msisahau ya kuwa Ekaristi ndiyo kiini cha imani. Yeye ndiye Mwanangu anayewalisheni kwa Mwili wake na kuwaimarisheni kwa Damu yake. Yeye ndiye ajabu ya upendo: Mwanangu ajaye tena mwenye uhai ili kuzifufua nafsi. Wanangu, mkiishi katika upendo, ninyi mnafanya mapenzi ya Mwanangu naye huishi ndani yenu. Wanangu, matakwa yangu ya kimama ni kwamba mpendeni zaidi na zaidi, maana Yeye anawapenda kwa upendo wake. Anawapa upendo wake ili muweze kuueneza kwa watu wote kandokando yenu. Kwa njia ya upendo wake, kama mama mimi nipo pamoja nanyi kuwaambieni maneno ya upendo na matumaini, kuwaambieni maneno ya milele na ya kushinda wakati na mauti, kuwaalikeni kuwa mitume wangu wa upendo. Nawashukuru! ”
“Wanangu wapendwa, ninawaalika kupokea kwa unyofu wa moyo maneno yangu, ninayowaambieni kama Mama ili muende katika njia ya mwanga kamili, wa usafi, wa upendo wa pekee wa Mwanangu, mtu na Mungu. Raha, mwanga usioelezeka kwa maneno ya kibinadamu utaingia nafsini mwenu, na mtashikwa na amani na upendo wa Mwanangu. Ninataka hayo kwa wanangu wote. Kwa hiyo ninyi, mitume wa upendo wangu, ninyi mnaojua kupenda na kusamehe, ninyi msiohukumu, ninyi ambao mimi ninahimiza, muwe mfano kwa wale wote wasiokwenda katika njia ya mwanga na upendo au waliotengana nayo. Kwa njia ya maisha yenu waonyesheni ukweli, waonyesheni upendo, maana upendo hushinda matatizo yote, na wanangu wote wana kiu ya upendo. Ushirika wenu wa upendo ni zawadi kwa Mwanangu na kwangu. Lakini, wanangu, kumbukeni ya kuwa kupenda maana yake ni kupenda mwenzako na kutakia wongofu wa nafsi yake. Ninapowatazama mmekusanyika karibu nami, moyo wangu unahuzunika kwa sababu ninaona upendo haba wa kidugu, upendo wenye huruma. Wanangu, Ekaristi, Mwanangu hai katikati yenu, na maneno yake yatawasaidia kuelewa. Neno lake, kweli, ni uhai, Neno lake huburudisha nafsi, Neno lake huwajulisha upendo. Wanangu wapenzi, ninawaombeni tena, kama Mama apendaye wana wake: wapendeni wachungaji wenu, waombeeni… Nawashukuru! ”
“Wanangu wapendwa, Mimi ni Mama wa ninyi nyote na kwa hiyo msiogope kwa sababu mimi ninasikia sala zenu, najua kwamba mnanitafuta na kwa hiyo ninamwomba Mwanangu kwa ajili yenu; Mwanangu ambaye yu katika mwuungo pamoja na Baba wa mbinguni na pamoja na Roho Mfariji, Mwanangu anayewaongoza roho katika Ufalme alikotoka, ambao ni Ufalme wa amani na wa mwanga. Wanangu, mmepewa uhuru wa kuchagua, kwa hiyo mimi kama Mama ninawasihi mchague uhuru kwa mema, na kwa moyo safi na mnyofu mnaelewa, ingawa pengine hamwelewi maneno yote, ndani yenu mng'amue ukweli ni nini. Wanangu, msipoteze ukweli na maisha ya kweli kwa kufuata maneno ya uongo. Kwa njia ya maisha ya kweli Ufalme wa mbinguni huingia katika mioyo yenu, ni Ufalme wa upendo, wa amani na wa maelewano. Katika Ufalme ule, wanangu, hautakuwa na ubinafsi wa kuwaondoa kutoka kwa Mwanangu, kutakuwa na upendo na maelewano na jirani yako. Kwa hiyo kumbukeni, ninawaambieni tena, kusali maana yake ni kuwapenda wengine, kumpenda jirani yako, kujitoa kwa ajili yao; pendeni na toeni kwa jina la Mwanangu, hapo Yeye atatenda kazi ndani yenu na kwa ajili yenu. Wanangu, fikirini daima juu ya Mwanangu, mpendeni bila kipimo na hapo mtakuwa na maisha ya kweli, yatakayokuwa ya milele. Nawashukuru enyi Mitume wa upendo wangu! ”
“Wanangu wapendwa, kwa upendo wa kimama ninawaalika kuifunua mioyo kwa imani, kuifunua mioyo kwa Mwanangu, ili katika mioyo yenu upendo kwa Mwanangu uimbe. Hakika, kutoka upendo huo tu, amani huingia nafsini. Wanangu, najua kwamba mna wema, najua kwamba mna upendo, upendo wenye rehema. Wanangu wangu wengi, lakini, wana moyo uliofungwa. Wanadhani kuweza kutenda pasipo kumwelekezea mawazo yao Baba wa mbinguni anayeangaza, pasipo kumwelekezea Mwanangu aliye daima pamoja nanyi katika Ekaristi na ataka kuwasikiliza. Wanangu, mbona hamzungumzi naye? Maisha ya kila mmoja wenu ni muhimu na ya thamani, maana ni zawadi ya Baba wa mbinguni kwa umilele. Kwa hiyo msisahau kamwe kumshukuru. Zungumzeni naye! Najua, enyi wanangu, ya kuwa mambo yatakayokuja hayajulikani kwenu lakini, mambo yenu ya mbele yatakapotokea, mtapata majibu yote. Upendo wangu wa kimama unataka muwe tayari. Wanangu, kwa maisha yenu wekeni katika mioyo ya watu mnaokutana hisia za amani, za mema, za upendo na msamaha. Kwa ajili ya sala, sikilizeni yanayowaambieni Mwanangu na tendeni namna hiyo. Ninawaalika tena kuwaombea wachungaji wenu, wale ambao Mwanangu aliwaita. Kumbukeni ya kuwa wanahitaji sala na upendo. Nawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa, maneno yangu ni manyofu lakini yamejaa upendo wa kimama na mahangaiko. Wanangu, juu yenu vivuli vya giza na vya udanganyifu vinaenea zaidi na zaidi, mimi ninawaiteni kuelekea mwanga na ukweli, mimi ninawaita kuelekea Mwanangu. Yeye peke yake huweza kugeuza kukata tamaa na maumivu yetu kuwa amani na utulivu, Yeye peke yake huweza kutoa matumaini katika maumivu makali sana. Mwanangu ni uzima wa ulimwengu, kwa kadiri mtakavyomjua, ndivyo mtakavyomkaribia na kumpenda maana Mwanangu ni upendo, na upendo unageuza yote. Yeye hufanya la ajabu hata neno lisilo la maana bila upendo machoni penu. Kwa hiyo nawaambieni tena ya kwamba mnapaswa kupenda sana ikiwa mnatamani kukua kiroho. Najua, enyi mitume wa upendo wangu, kwamba si rahisi sikuzote, lakini, wanangu, hata njia ngumu ni njia zinazoongoza kwenye ukuaji wa kiroho, wa kiimani na kwa Mwanangu. Wanangu, salini, mfikirie Mwanangu, nyakati zote za siku zenu inueni nafsi zenu kwake nami nitakusanya sala zenu kama maua kutoka bustani nzuri kuliko zote na kumpa Mwanangu. Muwe hakika mitume wa upendo wangu, wapeni wote upendo wa Mwanangu, muwe bustani zenye maua mazuri kuliko yote. Kwa njia ya sala saidieni wachungaji wenu ili waweze kuwa baba za kiroho waliojaa upendo kwa watu wote. Nawashukuru. ”
“Wanangu, ninawaomba kuwa hodari wala kutowayawaya, maana hata mema madogo zaidi, ishara ya upendo mdogo zaidi hushinda maovu yanayoonekana zaidi na zaidi. Wanangu nisikilizeni ili mema yashinde, ili muweze kujua upendo wa Mwanangu ulio furaha mkubwa zaidi kuliko zote. Mikono ya mwanangu inawakumbatia, Yeye, apendaye nafsi, Yeye ambaye amejitolea kwa ajili yenu na kunajitolea sikuzote tena katika Ekaristi, Yeye aliye na maneno ya Uzima wa milele; kujua upendo wake, kufuata hatua zake, maana yake ni kuwa na mali ya kiroho. Huo ni utajiri unaojaza hisia iliyo njema, na unaoona upendo na mema popote. Mitume wa upendo wangu, wanangu, muwe kama mionzi ya jua ambayo kwa joto la upendo wa Mwanangu inawapasha joto wote wale wanaoizunguka. Wanangu, ulimwengu unahitaji mitume wa upendo, ulimwengu unahitaji sala nyingi, lakini sala zinazosaliwa kwa moyo na roho, si kwa midomo tu. Wanangu, muwe na hamu ya utakatifu mkiwa na unyenyekevu unaomwezesha Mwanangu kufanya kazi kwa njia yenu, kama Yeye apendavyo. Wanangu, sala zenu, fikira zenu na matendo yenu, haya yote yawafungulia ama kuwafungia mlango wa Ufalme wa Mbinguni. Mwanangu aliwaonyesha njia na kuwapa tumaini, mimi ninawafariji na kuwapa moyo maana, wanangu, mimi nilijua maumivu, lakini nilikuwa na imani na tumaini, sasa nimepata thawabu ya uzima katika Ufalme wa Mwanangu. Kwa hiyo, nisikilizeni, jipeni moyo, msiwayawaye. Nawashukuru. ”
“Wanangu, Moyo wangu wa kimama unateseka wakati ninapotazama wanangu wasiopenda ukweli, wanaouficha; wakati ninapotazama wanangu wasiosali kwa moyo wala kwa matendo. Nimesikitika wakati ninapomwambia Mwanangu ya kuwa wana wangu wengi hawana imani tena, ya kuwa hawamjui Yeye, Mwanangu. Kwa hiyo ninawaalika, mitume wa upendo wangu: mjaribu kutazama mpaka ndani ya mioyo ya watu, na kule bila shaka mtapata hazina ndogo iliyofichwa. Kutazama hivyo ni rehema ya Baba wa mbinguni. Kutafuta mema hata palipo maovu makubwa zaidi, kutafuta kuwaelewana wala kutohukumiana: hilo ni neno ambalo Mwanangu anawaombeni. Nami, kama Mama, ninawaalika kumsikiliza. Wanangu, roho ni yenye nguvu kuliko mwili na, ikichukuliwa na upendo na matendo hushinda vikwazo vyote. Msisahau: Mwanangu aliwapendeni na anawapenda. Upendo wake ni pamoja nanyi na ndani yenu, wakati mpo kitu kimoja pamoja naye. Yeye ni mwanga wa ulimwengu, na hakuna mtu wala kitu kiwezacho kumsimamisha katika utukufu wa mwisho. Kwa hiyo, mitume wa upendo wangu, msiwe na hofu ya kushuhudia ukweli! Ushuhudieni kwa hamu, kwa matendo, kwa upendo, kwa sadaka yenu, lakini hasa kwa unyenyekevu. Shuhudieni ukweli kwa wale ambao hawajajua Mwanangu. Mimi nitakuwa karibu nanyi, mimi nitawatia moyo. Shuhudieni upendo usioishi tena, maana huja kutoka Baba wa mbinguni ambaye ni wa milele na anawatolea wana wangu wote umilele. Roho wa Mwanangu itakuwa karibu nanyi. Ninawaalika tena, wanangu: muwaombee wachungaji wenu, ombeni ili upendo wa Mwanangu uweze kuwaongoza. Nawashukuru. ”
“Wanangu, Wakati mnaponijia kama Mama kwa moyo safi na wazi, mjue ya kuwa ninawasikiliza, ninawatia moyo, ninawafariji na hasa ninawaombeeni kwa Mwanangu. Najua ya kuwa mnataka kuwa na imani thabiti na kuionyesha kwa njia inayofaa. Neno analotaka Mwanangu kutoka kwenu ni imani ya kweli, thabiti na kubwa. Hivyo kila njia mnavyoielezea ni ya kufaa. Imani ni fumbo la ajabu tunalohifadhi moyoni. Inakaa baina ya Baba wa Mbinguni na wana wake wote. Hutambulika kwa matunda na kwa upendo ambao sisi tunao kwa viumbe vyote vya Mungu. Enyi mitume wa upendo wangu, wanangu, mtumaini Mwanangu! Saidieni ili wanangu wote wajue upendo wake. Ninyi ni matumaini yangu, ninyi mnaojitahidi kupenda Mwanangu pasipo unafiki. Kwa jina la upendo, kwa wokovu wenu, kulingana na mapenzi ya Baba wa Mbinguni na kwa njia ya Mwanangu, nipo hapa katikati yenu. Mitume wa upendo wangu, kwa njia ya sala na sadaka mioyo yenu iangazwe na upendo na mwanga wa Mwanangu. Mwanga ule na upendo ule uangaze wote wale mnaokutana na uwarudishe kwa Mwanangu! Mimi nipo nanyi. Hasa nipo pamoja na wachungaji wenu: kwa upendo wangu wa kimama ninawaangaza na kuwatia moyo, ili, kwa njia ya mikono iliyobarikiwa na Mwanangu, wabariki ulimwengu mzima. Nawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa, inasikitisha kwamba katikati yenu, wanangu, yapo mashindano mengi, chuki, masilahi yenu wenyewe na ubinafsi. Wanangu, hivi kwa urahisi mnamsahau Mwanangu, maneno Yake na upendo Wake. Imani inazimika katika roho nyingi na mioyo imetekwa na vitu vya ulimwenguni. Lakini moyo wangu wa kimama unajua ya kuwa katikati yenu kuna wale wanaoamini na kupenda, wale ambao wanajaribu kumkaribia Mwanangu zaidi na zaidi, ambao wanamtafuta bila kuchoka na namna hii, wananitafuta hata mimi. Hawa ndio wanyenyekevu na wapole ambao, pamoja na maumivu na mateso wanayoyachukua katika kimya, pamoja na tumaini lao na hasa pamoja na imani yao, ni mitume wa upendo wangu. Wanangu, mitume wa upendo wangu, ninawafundisha ya kuwa Mwanangu hatafuti sala tu pasipo kuchoka bali hata matendo na hisia. Salini ili katika sala mpate kuzidi katika imani na katika upendo. Mpendane wenyewe kwa wenyewe: hilo ndilo analotaka Yeye, hiyo ndiyo ni njia ya uzima wa milele. Wanangu, msisahau ya kuwa Mwanangu ameleta mwanga kwa ulimwengu huu. Ameuleta kwa wale ambao walitaka kuuona na kuupokea. Hawa muwe ninyi, maana huu ndio mwanga wa ukweli, wa amani na wa upendo. Mimi ninawaongoza kama mama kumwabudu Mwanangu, kumpenda pamoja nami. Fikira zenu, maneno na matendo yenu yamwelekee Mwanangu, yawe katika jina Lake: hapo tu moyo wangu utajazwa. Nawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa, upendo na wema wa Baba wa mbinguni yanatoa mafunuo ili kwamba imani ikue, iweze kuelezwa, ilete amani, salama na matumaini. Hivi mimi nami, wanangu, kwa ajili ya upendo wenye rehema wa Baba wa mbinguni ninawaonyesha sikuzote tena njia ya kwenda kwa Mwanangu, kwa wokovu wa milele; kwa bahati mbaya, lakini, wanangu wengi hawataki kunisikiliza. Wanangu wengi wanasita. Lakini mimi, mimi, katika wakati na zaidi ya wakati, sikuzote nimemtukuza Bwana kwa mambo yale yote aliyoyatenda ndani yangu na kwa njia yangu. Mwanangu anajitolea kwenu, anamega mkate pamoja nanyi, anawaambieni maneno ya uzima wa milele ili muweze kuwaletea watu wote. Nanyi, wanangu, mitume wa upendo wangu, mnaogopa nini, ikiwa Mwanangu ni pamoja nanyi? Mwonyesheni nafsi zenu, ili Yeye aweze kuwa ndani yao na aweze kuwafanyeni kuwa vyombo vya imani, vyombo vya upendo. Wanangu, ishini Injili, ishini upendo wenye rehema kuelekea mwenzenu; lakini hasa ishini upendo kuelekea Baba wa mbinguni. Wanangu, hamkuungana kwa bahati tu. Baba wa mbinguni haunganishi watu kwa bahati tu. Mwanangu anaongea na nafsi zenu, nami ninaongea moyoni mwenu. Kama Mama ninawaambia: tembeeni nami! Pendaneni, na kutoa shuhuda! Hampasi kuogopa kulinda Ukweli, ambao ni Neno la Mungu, lililo la milele na lisilogeuka kamwe, kwa mifano yenu. Wanangu, yule anayetenda kazi katika mwanga wa upendo wenye rehema na ukweli, anasaidiwa sikuzote na Mbingu na hayuko peke yake. Mitume wa upendo wangu, waweze kuwatambua sikuzote katikati ya wengine wote katika maficho, upendo na utulivu wenu. Mimi nipo pamoja nanyi. Nawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa, ninawaita mitume wa upendo wangu. Ninawaonyesha Mwanangu, aliye amani ya kweli na upendo wa kweli. Kama Mama, kwa ajili ya neema ya kimungu, ninatamani kuwaongoza kwendea Yeye. Wanangu, kwa hiyo ninawaalika kujitazama ninyi wenyewe mkianzia kwa Mwanangu, kumtazama kwa moyo na kuona kwa moyo mahali mlipo na maisha yenu yanakwenda wapi. Wanangu, ninawaalika kuelewa ya kuwa mnaishi kwa ajili ya Mwanangu, kwa njia ya upendo wake na sadaka yake. Ninyi mnamwomba Mwanangu kuwa mwenye rehema nanyi, lakini mimi ninawaalika ninyi kuwa na rehema. Mnamwomba kuwa mwema nanyi na kuwasamehe, lakini tangu lini mimi ninawasihi ninyi, wanangu, kusamehe na kupenda watu wote mnaokutana nao! Mtakapoelewa kwa moyo maneno yangu, mtaelewa na kujua upendo wa kweli, na mtaweza kuwa mitume wa upendo ule, enyi mitume wangu, wanangu wapendwa. Nawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa, kama Mama ambaye anajua wana wake, ninajua ya kuwa mnamtamani Mwanangu. Ninajua ya kuwa mnatamani ukweli, amani, na kilicho chema wala si uovu. Kwa sababu hiyo mimi, kama Mama, kwa njia ya upendo wa Mungu ninawaita ninyi na kuwaalika ili, mkisali kwa moyo safi na wazi, mmtambue ninyi wenyewe Mwanangu, upendo wake, na Moyo wake wenye rehema. Mwanangu alikuwa akiona uzuri katika vitu vyote. Yeye anatafuta mema, hata yale mema madogo yanayofichika, katika roho zote, ili kusamehe maovu. Kwa hiyo, wanangu, mitume wa upendo wangu, ninawaalika kumwabudu, kumshukuru daima na kumstahili. Maana yeye aliwaambieni maneno ya kimungu, maneno ya Mungu, maneno yaliyo kwa watu wote na hata milele. Kwa hiyo, wanangu, ishini uchangamfu, umakini, umoja na muwe na mapenzi baina yenu. Haya mnapaswa kuwa nayo katika ulimwengu wa leo: hivyo mtakuwa mitume wa upendo wangu, hivyo mtashuhudia Mwanangu kwa jinsi ya haki. Nawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa, kwa upendo wa kimama ninawaalika ili kwa moyo safi na wazi, kwa imani kabisa, mpokee upendo mkubwa wa Mwanangu. Mimi ninajua ukuu wa upendo wake, mimi nilimchukua ndani yangu, Hostia moyoni, Mwanga na Upendo wa ulimwengu. Wanangu, hata kuelekea kwangu kwenu ninyi ni ishara ya upendo na ya huruma ya Baba wa Mbinguni, ni tabasamu kilichojaa upendo wa Mwanangu, ni mwaliko kwa uzima wa milele. Damu ya Mwanangu ilimwagika kwa ajili yenu kwa upendo. Ile Damu yenye thamani ni kwa wokovu wenu, kwa ajili ya uzima wa milele. Baba wa mbinguni aliumba mtu kwa ajili ya furaha ya milele. Haiwezekani ninyi kufa, ninyi mnaojua upendo wa Mwanangu, ninyi mnaomfuata. Uzima umeshinda: Mwanangu yu hai! Kwa hiyo, wanangu, mitume wa upendo wangu, sala iwaonyeshe njia, jinsi ya kueneza upendo wa Mwanangu kwa jinsi ilivyo bora zaidi. Wanangu, hata wakati mnapojaribu kuishi maneno ya Mwanangu, ninyi mnasali. Wakati mnapowapenda watu mnaokutana nao, mnaeneza upendo wa Mwanangu. Upendo ni neno linalofungua milango ya Uzima. Wanangu, tangu awali nimesali kwa ajili ya Kanisa. Kwa hiyo ninawaalika nanyi, mitume wa upendo wangu, kusali kwa ajili ya Kanisa na watumishi wake, kwa wale ambao Mwanangu amewaita. Nawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa, moyo safi na wazi tu utawawezesha ninyi kumjua kweli Mwanangu, na wale wote wasiojua upendo wake kuujua kwa njia yenu. Upendo tu utawawezesha kuelewa kuwa ni wenye nguvu kuliko kifo, maana upendo wa kweli umeshinda kifo na umefanya hata kifo hakipo tena. Wanangu, msamaha ni mtindo bora wa upendo. Ninyi, kama mitume wa upendo wangu, yawapasa kusali kwa kuwa wenye nguvu katika roho na kuweza kuelewa na kusamehe. Ninyi, mitume wa upendo wangu, kwa njia ya ufahamu na msamaha, mnatoa mfano wa upendo na rehema. Kuweza kuelewa na kusamehe ni karama inayotokana na maombi na yatupasa kuitunza. Mkisamehe ninyi mnaonyesha ya kuwa mnajua kupenda. Tazameni, wanangu, kama Baba wa mbinguni anavyowapenda kwa upendo mkubwa, kwa ufahamu, kwa uelewa, msamaha na haki. Kama anavyowatolea mimi, Mama wa mioyo yenu. Na tazama: mimi nipo katikati yenu ili kuwabariki kwa baraka ya kimama; ili kuwaalika kusali na kufunga; ili kuwasihi kuamini, kutumaini, kusamehe, kuwaombea wachungaji wenu na hasa kupenda bila mipaka. Wanangu, nifuateni! Njia yangu ni njia ya amani na upendo, njia ya Mwanangu. Ndiyo njia ya kuongoza katika ushindi wa Moyo wangu. Nawashukuru! ”
“Wanangu wapendwa, kufuatana na matakwa ya Baba mwenye rehema, nimewapa na tena nitawapa ishara dhahiri za uwepo wangu wa kimama. Wanangu, ishara hizo ni kwa hamu yangu ya kimama ya kuziponya roho. Ishara hizo ni kwa hamu ya kuwa kila mwanangu awe na imani ya kweli, aishi mang’amuzi ya ajabu akinywa kwenye chemchemi ya Neno la Mwanangu, Neno la uhai. Wanangu, kwa njia ya upendo wake na sadaka, Mwanangu alichukua ulimwenguni mwanga wa imani na aliwaonyesheni njia ya imani. Maana, wanangu, imani huamsha huzuni na maumivu. Imani ya kweli hufanya sala kusisika zaidi, hutimiza matendo ya huruma: mazungumzo na matoleo. Wale wanangu walio na imani, imani ya kweli, ni wenye heri pamoja na yote, maana wanaishi duniani mwanzo wa heri ya Mbinguni. Kwa hiyo, wanangu, mitume wa upendo wangu, ninawaalika kutoa mfano wa imani ya kweli, kupeleka mwanga pale palipo giza, kumwishi Mwanangu. Wanangu, kama Mama ninawaambia: hamwezi kupitia njia ya imani na kumfuata Mwanangu pasipo wachungaji wenu. Salini ili wawe na nguvu na upendo kwa kuwaongoza. Sala zenu ziwe sikuzote pamoja nao. Nawashukuru! ”
“Wanangu wapendwa, Upendo wa Mwanangu ni mkubwa. Laiti mngeweza kujua ukuu wa upendo Wake, msingeacha kamwe kumwabudu na kumshukuru. Yeye ni sikuzote hai pamoja nanyi katika Ekaristi, maana Ekaristi ni moyo Wake, Ekaristi ni moyo wa imani. Yeye hakuwaacha kamwe: hata wakati ninyi mlipojaribu kwenda mbali Naye, Yeye hakuwaacha kamwe.
Kwa hiyo, moyo wangu wa kimama unafurahi wakati unapotazama jinsi mlivyojaa upendo mnapomrudia, wakati unapoona ya kuwa mnamrudia kwa njia ya upatanisho, upendo na matumaini. Moyo wangu wa kimama unajua ya kuwa ikiwa mngetembea katika njia ya imani, mngekuwa kama machipukizi, kama matumba na kwa njia ya sala na kufunga mngekuwa kama matunda, kama maua, mitume wa upendo wangu, mngekuwa waleta mwanga na mngeangaza kwa upendo na hekima pande zote karibu nanyi.
Wanangu, kama mama, ninawaomba: salini, fikirini na kutafakari. Yote yanayowatokea, mazuri, ya kuumiza na ya kufurahisha, hayo yote yawasababisha kukua kiroho, yawafanya kuwa Mwanangu akue ndani yenu. Wanangu mkabidhi kwake. Mumwamini na mtumainie upendo Wake. Na Yeye awaongoze. Na Ekaristi iwe mahali mtakapolisha roho zenu ili kueneza upendo na ukweli. Shuhudieni Mwanangu. Ninawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa, Salini kila siku Tasbihi, taji lile la maua linaloniungana moja kwa moja kama Mama kwa maumivu yenu, mateso, mahitaji na matumaini. Mitume wa upendo wangu, Mimi nipo pamoja nanyi kwa njia ya neema na upendo wa Mwanangu, nanyi ninawaombeni sala. Sala zenu zinahitajika sana ulimwenguni, ili roho ziongoke! Fungueni wazi kwa imani timilifu mioyo yenu kwa Mwanangu, na yeye ataandika ndani yao muhtasari wa Neno lake, yaani upendo. Ishini muungano usiotenganika na Moyo Mtakatifu sana wa Mwanangu! Wanangu, kama Mama nawaambieni ya kwamba hakuna wakati wa kupoteza ili kupiga magoti mbele ya Mwanangu, kumkiri kama Mungu wenu, aliye kitovu cha maisha yenu. Mtoeni karama, zile anazozipenda zaidi, yaani upendo kwa jirani yako, rehema na mioyo safi. Mitume wa upendo wangu, wanangu wengi bado hawajamkiri Mwanangu kama Mungu wao, bado hawajajua upendo wake. Lakini ninyi, kwa njia ya sala yenu inayosema kwa moyo safi na wazi, pamoja na karama mnazotoa kwa Mwanangu, mtasababisha kwamba hata mioyo migumu zaidi ifunguke. Mitume wa upendo wangu, nguvu ya sala inayosemwa kutokana na moyo, ya sala yenye nguvu na iliyojaa upendo, hugeuza ulimwengu. Kwa hiyo, wanangu, salini, salini, salini! Mimi nipo pamoja nanyi.. Ninawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa, mapenzi na upendo wa Baba wa mbinguni hufanya mimi niwe katikati yenu, ili kusaidia kwa upendo wa kimama ukuaji wa imani katika mioyo yenu, ili kwamba muweze hakika kuelewa lengo la maisha ya kidunia na ukuu wa yale ya kimbingu. Wanangu, maisha ya kidunia ndiyo njia kuelekea umilele, kuelekea ukweli na uzima: kuelekea kwa Mwanangu. Kwa njia hii nataka kuwaongoza. Ninyi, wanangu, ninyi wenye sikuzote kiu ya upendo mkubwa zaidi, ukweli na imani, mjue ya kuwa moja tu ni chemchemi mnakoweza kunywa: imani katika Baba wa mbinguni, imani katika upendo wake. Mtegemee kabisa mapenzi yake wala msiogope: kila lililo bora kwa ajili yenu, kila linalowachukua kwenye uzima wa milele, mtapewa! Mtaelewa ya kuwa lengo la maisha si sikuzote kutaka na kutwaa, lakini kupenda na kutoa; mtakuwa na amani ya kweli na upendo wa kweli, mtakuwa mitume wa upendo. Kwa mfano wenu, mtawafanya wale wanangu wasiomjua Mwanangu na upendo wake watake kumjua. Wanangu, mitume wa upendo wangu, mwabuduni Mwanangu pamoja nami, na mpendeni juu ya vyote. Jaribuni sikuzote kuishi katika ukweli wake. Ninawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa, Mwanangu mpenzi alimwomba sikuzote na kumtukuza Baba wa Mbinguni. Sikuzote alikuwa amemwambia yote na kujiachia katika mapenzi yake. Hivyo mnapaswa kufanya hata ninyi, wanangu, maana Baba wa Mbinguni anawasikiliza sikuzote wanawe. Moyo wa umoja katika moyo mmoja: upendo, mwanga na uhai. Baba wa Mbinguni amejitolea kwa njia ya sura ya kibinadamu, na sura ile ndiyo sura ya Mwanangu. Ninyi, mitume wa upendo wangu, ninyi mnapaswa sikuzote kupokea sura ya Mwanangu katika mioyo yenu na katika fikira zenu. Ninyi mnapaswa sikuzote kuufikiria upendo wake na sadaka yake. Mnapaswa kusali ili kusudi mwone uwepo wake sikuzote. Maana, enyi mitume wa upendo wangu, hii ni jinsi ya kuwasaidia wale wote wasiomjua Mwanangu, wale ambao hawajajua upendo wake. Wanangu, someni kitabu cha Injili: ni sikuzote kitu kipya, ni kinachowaunganisha na Mwanangu, aliyezaliwa kwa kuwaletea maneno ya uzima wanangu wote na kwa kujitoa sadaka kwa ajili ya wote. Mitume wa upendo wangu, mkisukumwa na upendo kumwelekea Mwanangu, leteni upendo na amani kwa ndugu zenu wote. Msimhukumu mtu, pendeni kila mtu kwa njia ya upendo kwa kumwelekea Mwanangu. Hivyo mtashughulika hata na roho zenu, nayo ni yenye thamani kuliko kitu chochote mlicho nacho. Ninawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa, ninapowatazama ninyi mnaopenda Mwanangu, furaha inajaza Moyo wangu. Ninawabariki kwa baraka ya kimama. Pamoja na baraka ya kimama ninawabariki hata wachungaji wenu: ninyi mnaotangaza maneno ya Mwanangu, mnaobariki kwa mikono yake na mnaompenda hata kuwa tayari kufanya kwa furaha kila sadaka kwa ajili yake. Ninyi mfuateni Yeye, aliyekuwa Mchungaji wa kwanza, Mmisionari wa kwanza. Wanangu, mitume wa upendo wangu, kuishi na kufanya kazi kwa ajili ya wengine, kwa wale wote mnaopenda kwa njia ya Mwanangu, ni furaha na faraja ya maisha ya kidunia. Ikiwa kwa njia ya sala, upendo na sadaka Ufalme wa Mungu ni katika mioyo yenu, hapo kwa ninyi maisha ni yenye furaha na matulivu. Katikati ya wale wanaompenda Mwanangu na wanaopendana kwa ajili yake, maneno si ya lazima. Kutazamana kwatosha ili kusikia maneno yasiyonenwa na hisia zisizoonyeshwa. Pale panapotawala upendo, wakati hauna maana tena. Sisi ni pamoja nanyi! Mwanangu anawajua na kuwapenda. Upendo ni kilichowaongoza kwangu na, kwa njia ya upendo huu, mimi nitakuja kwenu na nitawaambieni kazi za wokovu. Ninataka ya kuwa wana wangu wote wawe na imani na wahisi upendo wangu wa kimama unaowaongoza kwa Yesu. Kwa hiyo ninyi, wanangu, ko kote mwendako angazeni kwa upendo na kwa imani, kama mitume wa upendo. Ninawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa, najua kuwepo katika maisha yenu na mioyo yenu. Nahisi upendo wenu, nasikia sala zenu na kuzipeleka kwa Mwanangu. Lakini, wanangu, mimi nataka kwa njia ya upendo wa kimama, kuwepo katika maisha ya wanangu wote. Nataka kukusanya karibu yangu wanangu wangu wote, chini ya joho langu la kimama. Kwa hiyo ninawaalika ninyi na kuwaiteni mitume wa upendo wangu, il mnisaidie. Wanangu, Mwanangu aliyatamka maneno haya: "Baba yetu”, Baba yetu uliye popote na katika mioyo yetu, kwa sababu ataka kuwafundisha kusali kwa maneno na kwa hisia zenu. Ataka muwe bora zaidi kila siku, muishi upendo wenye rehema ulio sala na sadaka isiyo na mipaka kwa ajili ya wengine. Wanangu mpeni Mwanangu upendo kwa jirani; mpeni jirani wenu maneno ya faraja, ya huruma na matendo ya haki. Yote mliyoyatoa kwa wengine, enyi mitume wa upendo wangu, Mwanangu anayapokea kama zawadi. Nami ni pamoja nanyi kwa sababu Mwanangu ataka kwamba upendo wangu, ulio kama mwali wa nuru, uzihuishe nafsi zenu, uwasaidie katika kutafuta amani na uheri wa milele. Kwa hiyo, wanangu, pendaneni, na muunganishwe kwa njia ya Mwanangu, ili muwe wana wa Mungu ambao wote pamoja kwa moyo uliojaa, wazi na safi mkisema kwa pamoja “Baba yetu” pasipo kuogopa! Ninawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa, nilichaguliwa kuwa mama wa Mungu na mama yenu, kwa maamuzi na upendo wa Bwana, lakini pia kwa mapenzi yangu, kwa upendo wangu usio na kifani kwake Baba wa mbinguni na kwa imani yangu yote Kwake. Mwili wangu ulikuwa kikombe cha Mungu Mtu. Nilikuwa mtumishi wa ukweli, wa upendo na wokovu kama vile nilivyo sasa katikati yenu, ili kuwaalika, wanangu, mitume wa upendo wangu, kuwa waletaji ukweli, ili kuwaalika, kwa njia ya utashi na upendo yenu kumwelekea Mwanangu, ili kueneza maneno Yake, maneno ya wokovu na kuyaonyesha, kwa vitendo vyenu, kwa wale wote ambao hawajamjua mwanangu na upendo Wake. Nguvu mtaipata katika Ekaristi: Mwanangu awalisheni kwa mwili Wake na kuwaimarisha kwa damu Yake. Wanangu, wekeni mikono yenu pamoja kwa sala na tazameni kuelekea msalaba kwa ukimya. Kwa jinsi hii mtapata imani ili muweze kuieneza, mtapata ukweli ili muweze kuupambanua, mtapata upendo ili muweze kuelewa namna ya kupenda kwa uhakika. Wanangu, mitume wa upendo wangu, wekeni mikono yenu pamoja kwa sala na tazameni kuelekea msalaba: katika msalaba tu kuna wokovu. Ninawashukuru. ”
“Wanangu wapendwa, upendo wenu safi na wa kweli unavuta Moyo wangu wa kimama. Imani yenu na usadiki wenu katika Baba wa mbinguni ni mawaridi yenye harufu nzuri mnayonitolea: shada la mawaridi mazuri sana, lililotengenezwa kwa sala zenu, kwa matendo ya rehema na ya upendo. Mitume wa upendo wangu, ninyi mnaojaribu kumfuata Mwanangu pasipo unafiki na kwa moyo safi, ninyi ambao pasipo unafiki mnampenda, muwe ninyi wenyewe kusaidia: muwe mfano kwa wale ambao hawajajua upendo wa Mwanangu. Lakini, wanangu, siyo kwa maneno tu, bali hata kwa matendo na hisia safi, ambayo kwa njia yake mnamtukuza Baba wa mbinguni. Mitume wa upendo wangu, ni wakati wa kukesha na ninawaombeni upendo; na msihukumu mtu yeyote, kwa maana Baba wa mbinguni atahukumu wote. Ninawaombeni mpende, na mueneze ukweli, kwa maana ukweli ni wa kale: Ukweli siyo mpya, Ukweli ni wa milele, Ukweli ndiyo ukweli! Ukweli unatolea ushuhuda wa umilele wa Mungu. Bebeni mwanga wa Mwanangu na mpasue giza ambalo linataka kuwakandamiza zaidi na zaidi. Msiwe na hofu: kwa ajili ya neema na upendo wa Mwanangu, mimi nipo pamoja nanyi! Ninawashukuru. ””
To compare Medjugorje messages with another language versions choose