Language 

Updates  | Medjugorje[EN]  | Messages  | News & Articles[EN]  | Videos[EN]  | Pictures & Photos[EN] | Site Map  | About[EN]

www.medjugorje.ws » PDA version » Our Lady of Medjugorje Messages » Our Lady of Medjugorje Messages

Our Lady of Medjugorje Messages

Wanangu wapendwa, Leo ninawaalika kusali tena zaidi ili msikie katika mioyo yenu utakatifu wa msamaha. Katika familia lazima kuwepo utakatifu kwa sababu enyi wanangu, ulimwengu hauna wakati ujao bila upendo na utakatifu, kwa sababu katika utakatifu na katika furaha ninyi mjitolee kwa Mungu Mwumbaji anayewapendeni kwa upendo mkubwa sana. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa, najua kuwepo katika maisha yenu na mioyo yenu. Nahisi upendo wenu, nasikia sala zenu na kuzipeleka kwa Mwanangu. Lakini, wanangu, mimi nataka kwa njia ya upendo wa kimama, kuwepo katika maisha ya wanangu wote. Nataka kukusanya karibu yangu wanangu wangu wote, chini ya joho langu la kimama. Kwa hiyo ninawaalika ninyi na kuwaiteni mitume wa upendo wangu, il mnisaidie. Wanangu, Mwanangu aliyatamka maneno haya: "Baba yetu”, Baba yetu uliye popote na katika mioyo yetu, kwa sababu ataka kuwafundisha kusali kwa maneno na kwa hisia zenu. Ataka muwe bora zaidi kila siku, muishi upendo wenye rehema ulio sala na sadaka isiyo na mipaka kwa ajili ya wengine. Wanangu mpeni Mwanangu upendo kwa jirani; mpeni jirani wenu maneno ya faraja, ya huruma na matendo ya haki. Yote mliyoyatoa kwa wengine, enyi mitume wa upendo wangu, Mwanangu anayapokea kama zawadi. Nami ni pamoja nanyi kwa sababu Mwanangu ataka kwamba upendo wangu, ulio kama mwali wa nuru, uzihuishe nafsi zenu, uwasaidie katika kutafuta amani na uheri wa milele. Kwa hiyo, wanangu, pendaneni, na muunganishwe kwa njia ya Mwanangu, ili muwe wana wa Mungu ambao wote pamoja kwa moyo uliojaa, wazi na safi mkisema kwa pamoja “Baba yetu” pasipo kuogopa! Ninawashukuru.
Wanangu wapendwa, Nawaletea ninyi Mwanangu Yesu ili awabariki na kuwafunulia Upendo wake utokao mbinguni. Moyo wenu unatamani amani inayopungua zaidi na zaidi duniani. Kwa sababu hiyo watu wako mbali na Mungu, nafsi zinaumwa na zinaelekea kifo cha kiroho. Mimi nipo pamoja nanyi, wanangu, niwaongoze kwenye njia hii ya wokovu ambayo Mungu anawaiteni. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa, ninapowatazama ninyi mnaopenda Mwanangu, furaha inajaza Moyo wangu. Ninawabariki kwa baraka ya kimama. Pamoja na baraka ya kimama ninawabariki hata wachungaji wenu: ninyi mnaotangaza maneno ya Mwanangu, mnaobariki kwa mikono yake na mnaompenda hata kuwa tayari kufanya kwa furaha kila sadaka kwa ajili yake. Ninyi mfuateni Yeye, aliyekuwa Mchungaji wa kwanza, Mmisionari wa kwanza. Wanangu, mitume wa upendo wangu, kuishi na kufanya kazi kwa ajili ya wengine, kwa wale wote mnaopenda kwa njia ya Mwanangu, ni furaha na faraja ya maisha ya kidunia. Ikiwa kwa njia ya sala, upendo na sadaka Ufalme wa Mungu ni katika mioyo yenu, hapo kwa ninyi maisha ni yenye furaha na matulivu. Katikati ya wale wanaompenda Mwanangu na wanaopendana kwa ajili yake, maneno si ya lazima. Kutazamana kwatosha ili kusikia maneno yasiyonenwa na hisia zisizoonyeshwa. Pale panapotawala upendo, wakati hauna maana tena. Sisi ni pamoja nanyi! Mwanangu anawajua na kuwapenda. Upendo ni kilichowaongoza kwangu na, kwa njia ya upendo huu, mimi nitakuja kwenu na nitawaambieni kazi za wokovu. Ninataka ya kuwa wana wangu wote wawe na imani na wahisi upendo wangu wa kimama unaowaongoza kwa Yesu. Kwa hiyo ninyi, wanangu, ko kote mwendako angazeni kwa upendo na kwa imani, kama mitume wa upendo. Ninawashukuru.
Wanangu wapendwa, wakati huu uwe kwenu wakati wa sala. Bila Mungu hamwezi kuwa na amani. Kwa hiyo, wanangu, salini kwa ajili ya amani katika mioyo yenu na katika familia zenu ili Yesu aweze kuzaliwa ndani yenu na kuwapeni upendo wake na baraka yake. Ulimwengu uko katika vita kwa sababu mioyo imejaa machukio na wivu. Wanangu, wasiwasi unaonekana katika macho yenu kwa sababu hamkuruhusu Yesu kuzaliwa katika maisha yenu. Mtafuteni, ombeni na Yeye atajitoa kwenu katika yule Mtoto aliye furaha na amani. Mimi niko pamoja nanyi na ninasali pamoja nanyi. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa, Mwanangu mpenzi alimwomba sikuzote na kumtukuza Baba wa Mbinguni. Sikuzote alikuwa amemwambia yote na kujiachia katika mapenzi yake. Hivyo mnapaswa kufanya hata ninyi, wanangu, maana Baba wa Mbinguni anawasikiliza sikuzote wanawe. Moyo wa umoja katika moyo mmoja: upendo, mwanga na uhai. Baba wa Mbinguni amejitolea kwa njia ya sura ya kibinadamu, na sura ile ndiyo sura ya Mwanangu. Ninyi, mitume wa upendo wangu, ninyi mnapaswa sikuzote kupokea sura ya Mwanangu katika mioyo yenu na katika fikira zenu. Ninyi mnapaswa sikuzote kuufikiria upendo wake na sadaka yake. Mnapaswa kusali ili kusudi mwone uwepo wake sikuzote. Maana, enyi mitume wa upendo wangu, hii ni jinsi ya kuwasaidia wale wote wasiomjua Mwanangu, wale ambao hawajajua upendo wake. Wanangu, someni kitabu cha Injili: ni sikuzote kitu kipya, ni kinachowaunganisha na Mwanangu, aliyezaliwa kwa kuwaletea maneno ya uzima wanangu wote na kwa kujitoa sadaka kwa ajili ya wote. Mitume wa upendo wangu, mkisukumwa na upendo kumwelekea Mwanangu, leteni upendo na amani kwa ndugu zenu wote. Msimhukumu mtu, pendeni kila mtu kwa njia ya upendo kwa kumwelekea Mwanangu. Hivyo mtashughulika hata na roho zenu, nayo ni yenye thamani kuliko kitu chochote mlicho nacho. Ninawashukuru.
Wanangu wapendwa, Leo ninawaalika kusali. Sala iwe manukato kwa roho zenu kwani tunda la sala ni furaha, kutoa, kumshuhudia Mungu kwa wengine kwa njia ya maisha yenu. Wanangu, mkimtegemea Mungu kabisa, Yeye atashughulika yote, atawabariki na sadaka zenu zitapata maana. Mimi nipo pamoja nanyi na ninawabariki nyote kwa baraka yangu ya kimama. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa, mapenzi na upendo wa Baba wa mbinguni hufanya mimi niwe katikati yenu, ili kusaidia kwa upendo wa kimama ukuaji wa imani katika mioyo yenu, ili kwamba muweze hakika kuelewa lengo la maisha ya kidunia na ukuu wa yale ya kimbingu. Wanangu, maisha ya kidunia ndiyo njia kuelekea umilele, kuelekea ukweli na uzima: kuelekea kwa Mwanangu. Kwa njia hii nataka kuwaongoza. Ninyi, wanangu, ninyi wenye sikuzote kiu ya upendo mkubwa zaidi, ukweli na imani, mjue ya kuwa moja tu ni chemchemi mnakoweza kunywa: imani katika Baba wa mbinguni, imani katika upendo wake. Mtegemee kabisa mapenzi yake wala msiogope: kila lililo bora kwa ajili yenu, kila linalowachukua kwenye uzima wa milele, mtapewa! Mtaelewa ya kuwa lengo la maisha si sikuzote kutaka na kutwaa, lakini kupenda na kutoa; mtakuwa na amani ya kweli na upendo wa kweli, mtakuwa mitume wa upendo. Kwa mfano wenu, mtawafanya wale wanangu wasiomjua Mwanangu na upendo wake watake kumjua. Wanangu, mitume wa upendo wangu, mwabuduni Mwanangu pamoja nami, na mpendeni juu ya vyote. Jaribuni sikuzote kuishi katika ukweli wake. Ninawashukuru.
Wanangu wapendwa, Leo ninawaalika kusali kwa ajili ya makusudi yangu ili niweze kuwasaidia. Wanangu, salini Rosari mkitafakari mafumbo ya Rosari maana hata ninyi katika maisha yenu mnapitia furaha na maumivu. Kwa njia hii mtageuza mafumbo katika maisha yenu maana maisha ni fumbo hadi mtakapoyaweka katika mikono ya Mungu. Hivyo mtakuwa na mang'amuzi ya imani kama Petro aliyemkuta Yesu na Roho Mtakatifu aliyoijaza roho yake. Hata ninyi, wanangu, mnaalikwa kushuhudia mkiishi upendo ambao kwao siku kwa siku Mungu anawajaza kwa njia ya uwepo wangu. Kwa hiyo, wanangu, muwe wazi na salini kwa moyo katika imani. Asanteni kwa kuitikia wito wangu.
Wanangu wapendwa, Salini kila siku Tasbihi, taji lile la maua linaloniungana moja kwa moja kama Mama kwa maumivu yenu, mateso, mahitaji na matumaini. Mitume wa upendo wangu, Mimi nipo pamoja nanyi kwa njia ya neema na upendo wa Mwanangu, nanyi ninawaombeni sala. Sala zenu zinahitajika sana ulimwenguni, ili roho ziongoke! Fungueni wazi kwa imani timilifu mioyo yenu kwa Mwanangu, na yeye ataandika ndani yao muhtasari wa Neno lake, yaani upendo. Ishini muungano usiotenganika na Moyo Mtakatifu sana wa Mwanangu! Wanangu, kama Mama nawaambieni ya kwamba hakuna wakati wa kupoteza ili kupiga magoti mbele ya Mwanangu, kumkiri kama Mungu wenu, aliye kitovu cha maisha yenu. Mtoeni karama, zile anazozipenda zaidi, yaani upendo kwa jirani yako, rehema na mioyo safi. Mitume wa upendo wangu, wanangu wengi bado hawajamkiri Mwanangu kama Mungu wao, bado hawajajua upendo wake. Lakini ninyi, kwa njia ya sala yenu inayosema kwa moyo safi na wazi, pamoja na karama mnazotoa kwa Mwanangu, mtasababisha kwamba hata mioyo migumu zaidi ifunguke. Mitume wa upendo wangu, nguvu ya sala inayosemwa kutokana na moyo, ya sala yenye nguvu na iliyojaa upendo, hugeuza ulimwengu. Kwa hiyo, wanangu, salini, salini, salini! Mimi nipo pamoja nanyi.. Ninawashukuru.
To compare Medjugorje messages with another language versions choose
<<Previous  1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 11 ... 23 Next>>

 

PC version: This page | Medjugorje | Apparitions[EN]  | Our Lady of Medjugorje Messages  | Medjugorje News & Articles[EN]  | Pictures & Photos[EN]  | Medjugorje Videos[EN]